David Haye ajiandaa kutangaza kustaafu

David Haye Haki miliki ya picha AFP
Image caption David Haye

Bingwa zamani wa masumbwi uzito wa juu David Haye anajiandaa kutangaza kustaafu mchezo huo.

Bondia huyo mkaazi wa London ameifahamisha Bodi la kudhibiti mchezo wa Ndondi nchini Uingereza, kwamba hakusudi kutengeneza upya leseni yake.

Haye, ambaye atafikisha umri wa miaka 31 siku ya Alhamisi, mara kwa mara amesema asingependa kuendelea na mchezo huo akishavuka umri wa miaka 30.

Hata hivyo, wengi wanatumai Haye atachelewesha uamuzi wake kwa takriban pambano moja kubwa na hasa dhidi ya Vitali Klitschko.

Pambano lake la mwisho dhidi ya Wladimir Klitschko mwezi wa Julai alichapwa kwa pointi na kupoteza mkanda wake wa ubingwa wa dunia wa WBA mjini Hamburg.

Mara nyingi Haye amekuwa akihusishwa na mpambano dhidi ya Vitali, anayeshikilia mkanda wa ubingwa wa dunia wa WBC.