Bi Sirleaf aridhia duru ya pili Liberia

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Bi Sirleaf

Rais wa Liberia Ellen Johnson-Sirleaf amesema ameridhia kukabiliana na duru ya pili ya uchaguzi dhidi ya aliyekuwa mwanadiplomasia wa umoja wa mataifa Winston Tubman.

Huku takriban kura zote zikiwa zimeshahesabiwa, Bi Sirleaf alipata kura nyingi zaidi lakini alishindwa kuvuka asilimia 50 inayotakiwa kupata ushindi.

Bw Tubman alisema atagombea tena katika duru hiyo baada ya chama chake kudai kuwepo udanganyifu na kudai kujitoa.

Huu ni uchaguzi wa pili Liberia tangu kumalizika kwa miaka 14 ya vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 2003.

Bi Sirleaf, ambaye alipewa tuzo ya amani ya Nobel wiki iliyopita, alishinda uchaguzi wa mwaka 2005 na kuwa mwanamke wa kwanza Mwafrika kuchaguliwa kuwa rais.

Alimshinda aliyekuwa mcheza soka George Weah, ambaye kwa sasa ni mgombea mwenza wa Bw Tubman.

Bi Sirleaf alisema yuko tayari kwa ushindani lakini pia alikuwa ana uhakika wa kushinda.

Ikiwa aslimia 96 ya kura zote zikiwa zimehesabiwa, yeye ana asilimia 44 dhidi ya 32 za Bw Tubman, tume ya uchaguzi imetangaza. Waliojitokeza kupiga kura ni asilimia 74.

"Duru ya pili ni karibu sana," alisema James Fromayah kutoka tume ya taifa ya uchaguzi (NEC). Imepangwa kufanyika Novemba 8.