West Ham kuwania uwanja Olimpiki

Uwanja wa Olimpiki wa London
Image caption Uwanja wa Olimpiki wa London

Makamu mwenyekiti wa West Ham United Karren Brady, amesema klabu hiyo ya soka bado inakusudia kuhamia uwanja wa Olimpiki itakapofika mwaka 2014.

West Ham ilionekana kufanikiwa kupata nafasi ya kukabidhiwa uwanja huo kufuatia michezo ya Olimpiki ya London mwaka 2012.

Lakini uwanja huo, uliogharimu zaidi ya paundi milioni 500 kuujenga, kwa sasa utaendelea kuwa chini ya umiliki wa umma.

Bodi ya uwanja wa huo wa Olimpiki (OPLC) imeamua kumaliza mazungumzo na West Ham kwa sababu ya kucheleweshwa masuala ya kisheria.

Bodi hiyo ya OPLC imefanya uamuzi huo baada mazungumzo na Meya wa London pamoja na serikali, ambapo imeweka wazi msimamo huo kupitia taarifa iliyotolewa na Idara ya Utamaduni, Habari na Michezo.

"Uwanja kwa sasa utashikiliwa kama mali ya umma na OPLC wametakiwa kuanza mchakato mpya kwa ajili ya kupata wapangaji katika uwanja huo."

Katika taarifa ya pamoja Kim Bromley-Derry, mtendaji mkuu wa Baraza la Mji wa Newham, Brady amesema West Ham watahitaji kuwa wapangaji wa uwanja huo wakati mchakato wa kutangaza tenda utakapofunguliwa upya na watabakisha sehemu ya kandanda na riadha pamoja.