Huwezi kusikiliza tena

Kisa na Mkasa na Salim Kikeke

KAUZA MTOTO

Haki miliki ya picha spl
Image caption Mtoto kauzwa (sio huyu)

Polisi nchini Uchina wanamsaka mtu mmoja ambaye aliamua kumuuza mtoto wake wa kiume, baada ya kugombana na mke wake.

Mtoto huyo aliuzwa kwa dola elfu tano. Kwa mujibu wa BBC mke wa bwana huyo anayefanya katika mji mwingine alianza kumkabili mume wake huyo ambaye ni mvivu na asiyependa kufanya kazi.

Bwana huyo alimsubiri mkewe aende kazini na kisha kumchukua mtoto wao na kumuuza kwa familia nyingine. Mama wa mtoto huyo aligundua kuwa mwanaye ameuzwa aliporejea miezi kadhaa baadaye.

Mama huyo alimtafuta mwanae na kumpata, ingawa familia iliyomnunua mtoto awali iligoma kumrejesha kwa madai kuwa walikuwa wametia saini mkataba wa mauzo.

Hatimaye familia hiyo ilikubali kumrejesha mtoto huyo baada ya kurudishiwa dola zao elfu tano. Baba wa mtoto huyo amekimbilia mafichoni.

Familia zilizohusika na sakata hilo zimegoma kuzungumza na waandishi wa habari. Polisi pia wamekataa kusema lolote, na mwandishi wa BBC aliambiwa na polisi hao-- Usitangaze kisa hiki, kitatoa picha mbaya ya Uchina-- amenukuliwa polisi mmoja akisema.

PAKA NDANI YA FRIJI

Haki miliki ya picha PA
Image caption Paka

Bwana mmoja nchini New Zealand amekutwa akiishi na paka wapatao sitini nyumbani kwani.

Hata hivyo kwa sasa anakabiliwa mashataka ya kutesa wanyama, baada ya paka wengine wapatao 38 kukutwa wamekufa na kuhifadhiwa ndani ya friji lake.

Bwana huyo Donald Cruickshank mwenye umri wa miaka 77, anadaiwa kuhifadhi mizoga paka hao kwa kuifunga na vipande vya magazeti, na kuweka karibu na sehemu anayoweka chakula chake, ndani ya friji.

Shirika la dhamana ya wanyama SPCA limesema maafisa wake walikuta paka 19 wakirandaranda ndani ya nyumba ya bwana huyo, wengine 17 walikuwa wamefungiwa, na paka wengine 23 wakiwa katika ghorofa la chini katika hali mbaya ya kiafya.

Bwana huyo, ambaye amekana mashtaka yake ameliambia gazeti la Herald kuwa aliwahifadhi paka hao ndani ya freezer lake kwa takriban miaka mitatu, kwa sababu hakuwa na muda wa kuwazika.

MWANARIADHA MPANDA BASI

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Marathon

Mwanariadha mmoja nchini Uingereza, amevuliwa medali ya shaba aliyopewa baada ya kumaliza mbio hizo katika nafasi ya tatu na katika mbio hizo za kilomita arobaini na mbili.

Mwanariadha huyo Rob Sloan alivuliwa medali hiyo baada ya kugunduliwa kuwa alipanda basi lililompeleka hadi mstari wa kumaliza mbio.

Awali wakati akikabidhiwa medali yake, wakimbiaji wenzake walianza kuulizana na kushangazwa walipitwa saa ngapi na mwenzao huyo. Alipoulizwa, mwanzo alikana kufanya kosa lolote, ingawa baadaye bwana huyo alikiri kuwa alipanda basi baada kujisikia mchovu.

Amesema basi hilo lilimpeleka hadi karibu na mwisho wa mbio, ambapo alijificha na kusubiri mtu wa kwanza na wa pili kumaliza mbio, na yeye kujitokeza na kujifanya amemaliza katika nafasi ya tatu.

Watu walioshuhudia wamesema walimuona akiwa amejificha nyuma ya mti, mpaka alipoona mshindi wa kwanza na wa pili wakimaliza, na yeye kuungana nao katika nafasi ya tatu.

PEPO YA POMBE

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Kinywaji

Bwana mmoja nchini Marekani amesema alidhani amekufa na kwenda peponi. Bwana huyo wa mjini Illinois, amewaambia polisi kuwa alidhani kuwa yuko peponi baada ya kukuta gari lililokuwa limebeba pombe likiwa limeegeshwa barabarani likiwa halina mtu.

Bwana huyo alianza kugida pombe hizo bila kipimo.

Polisi wa Illinois wameliambia gazeti la Trib kuwa bwana huyo alikutwa amelewa chakari, baada ya kunywa bia hizo siku ya Jumanne.

Watu walioshihudia tukio hilo waliita polisi na gari la kubebea wagonjwa kutokana na kulewa mno kwa mtu huyo. Bwana huyo amewaambia polisi kuwa hajafanya kosa lolote, na hakuna mashtaka yoyote yamefunguliwa dhidi yake.

MWIZI NJAA

Haki miliki ya picha none
Image caption Mwivi

Mwizi mmoja nchini Uchina alikutwa akikaribia kufa, baada ya kufungiwa ndani ya nyumba aliyopanga kufanya wizi wake kwa siku nne.

Mtandao wa Shangai Daily umesema mwizi huyo alinyata na kuingia kimya kimya katika nyumba moja baada ya kukuta mlango uko wazi.

Mwizi huyo aliyetambulika kwa jina moja tu la He, anatuhumiwa kuingia katika nyumba hiyo iliyopo kwenye ghorofa ya sita katika jiji la Taicang lililopo katika jimbo la Jiangsu, mashariki mwa Uchina.

Mwizi huyo alijificha katika chumba kingine na kusubiri mwenye nyumba aondoke ili aanze kuiba vilivyondani ya nyumba hiyo, kimeripoti kituo cha TV cha Anhui. Mwenye nyumba huyo aliondoka, lakini akafunga mlango wa nyumba kwa nje.

Mwizi huyo alivunjika moyo baada ya kukuta hakuna chakula ndani ya nyumba. Alizidi kupagawa baada ya simu yake kuisha betri ba hakuwa na chaja, na hivyo kushindwa hata kupiga simu kuomba msaada. Mwenye nyumba aliporejea siku nne baadaye, alimkuta mwizi huyo akipumua kwa taabu, na hakuweza hata kusimama mwenyewe.

Mwenye nyumba huyo aliita polisi na mwizi huyo kupelekwa korokoroni.

SAFINA

Bwana mmoja katika jimbo la kati ya Henan nchini Uchina, anaamini kuwa dunia itakumbwa na gharika na kufikia mwisho wake mwaka 2012, na hivyo ameamua kuajiri watu kujenga safina yake mwenyewe.

Safina hiyo inayogharimu dola elfu tatu za kimarekani, inajengwa kwa kutumia tenki la zamani la mafuta lenye kipenyo cha mita mbili na nusu katika jiji la Luohe.

Safina hiyo ina njia tatu za kupitisha hewa, madirisha kadhaa madogo na pia imewekewa matairi sita, na hivyo inaweza kuvutwa na gari, umeripoti mtandao wa Dahe.com.

Siku ya siku itakapofika, tenki hilo litaelea juu ya maji, na milango na madirisha yatafungwa kithabiti kabisa, imesema taarifa hiyo ya Dahe.com.

Safina hiyo itakuwa na uwezo wa kubeba watu ishirini na itakuwa na vyumba vitatu. Chumba cha kwanza kitakuwa choo, cha pili cha kuhifadhia vitu, yaani stoo ambayo itakuwa na uwezo wa kuhifadhi chakula cha mwezi mmoja, na chumba cha tatu kitakuwa cha kulala.

Wafanyakazi wanaojenga safina hiyo wamesema pia wataweza air condition ndani, pamoja na jenereta na vifaa vya jikoni.

Na kwa taarifa yako....

Saa zilizotengenezwa kabla ya mwaka 1660 zilikuwa na mshale mmoja tu, wa saa, bila ya ule wa dakila.

Tukutane wiki Ijayo, panapo majaaliwa.