Zanzibar yatoa mwongozo wa uzazi

Zanzibar
Image caption Zanzibar

Katika juhudi za kupunguza kiwango cha uzazi huko Zanzibar, Serikali ya Visiwa hivyo kwa kutumia wataalamu imetengeneza mwongozo unao shawishi wananchi wake kupunguza kiwango cha uzazi.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Uzazi wa Mpango katika Wizara ya Afya Dk Hanuni Wazir mpango huo umelenga kutumia hoja za dini ya Kiislamu kushawishi watu wenye umri wa kupata watoto kupunguza idadi ya watoto wanaozaa.

Kwa mujibu wa sensa ya taifa iliofanyika miaka 10 iliyopita idadi ya wananchi wa Zanzibar hivi sasa ni milioni moja na laki moja na kiwango cha uzazi ni cha wastani wa 5.1 kwa mujibu wa utafiti uliofanywa mwaka 2007.

Dk Hanuni amesema baada ya juhudi mbali mbali kuelimisha umma juu ya athari ya idadi ya watu katika suala la kupanga maendeleo lakini pia kwa usalama na afya ya mama.

“Tunataka lengo letu tufikie wastani wa asilimia 4. Kila mwanamke anaeweza kuzaa azae watoto wasiozidi wanne.”

Mwandishi wetu wa Zanzibar Ally Saleh Albarto anasema kuwa wakaazi wa Visiwa hivyo hutumia hoja za kidini kudai kuwa hakuna maagizo yoyote ya kidini kufanya uzazi wa mpango.

“Tumekusanya watalamu wa kidini wakiongozwa na kutafuta maoni yao na hatimae Dk. Issa Ziddy ameandika kitabu ambacho kimetoa hoja nyingi za kwa nini uislamu unahimiza uzazi wa majira,” amesema Dk Hanuni.

“Kilichofanywa ni kuchukua hoja mbali mbali za kiislamu na kuziweka pamoja ili kila shekhe na kila imamu atumie membari kushawishi waumini kwa vile asilimia 85 ya watu wake ni Waislamu,” amseme Dk Hanuni.

Kitabu hicho kimeandikwa kwa lugha ya Kiswahili na kitatawanywa maeneo mbali mbali ili kuhimiza uzazi huo wa majira kwa nguzo ya Kiislamu