Mutassim Gaddafi 'akamatwa' mjini Sirte

Kumekuwa na taarifa za kuhitilafiana kuhusu mmoja wa wanawe Kanali Gaddafi, Muttasim, ambaye alihudumu kama mshauri mkuu wa usalama wa kitaifa katika serikali ya babake.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Habari hizi zimevutia raia wengi

Afisa mmoja wa baraza la mpito la kitaifa (NTC) amesema kuwa Mutassim Gaddafi amekamatwa mjini Sirte na kupelekwa Benghazi japo mwengine kutoka baraza hilo hilo amesema kuwa habari hizo haziwezi kuthibitishwa.

Lakini licha ya hilo raia wa Libya mjini Benghazi na hata Tripoli wamekuwa wakisherehekea.

Taarifa zinadai kuwa Mutassim alikamatwa akiwa kwenye harakati za kutoroka kutoka mjini Sirte ambao umeshuhudia mapigano makali kati ya wanajeshi wa NTC na wale watiifu kwa Kanali Gaddafi.

Wakuu wa jeshi la NTC wanasema sasa hivi wanadhibiti eneo kubwa la mji huo wa Sirte.

Ikiwa kweli Mutassim Gaddafi atakuwa amekamatwa, hii itakuwa habari njema kwa baraza la mpito na pigo kwa makundi yaliyosalia yanayomtii Kanali Gaddafi.

Inadaiwa kuwa wanajeshi waliokuwa wakipigana na wale wa baraza la NTC mjini Sirte alipozaliwa Kanali Gaddafi wamekuwa wakimlinda Mutassim.

Ikiwa ni kweli amekamatwa, Mutassim atakuwa mtu wa kwanza kwenye ukoo wa Gaddafi kushikwa.

Mke wa Kanali Gaddafi na watoto wake wa kike wapo nchini Algeria na kaka yake Saif al Islam anadaiwa kuwa mafichoni mjini Bani Walid.

Raia wengi wa Libya wanaounga mapinduzi haya wanahamu kuona Kanali Gaddafi ameshikwa akiwa hai.