Marekani imetuma wanajeshi Uganda

Wanajeshi kama 100 wa Marekani wametumwa Uganda kusaidia katika shughuli za kuwasaka wapiganaji wa LRA, kikundi kinachotuhumiwa kuvunja sana haki za kibinaadamu nchini Uganda pamoja na nchi za jirani, kwa miongo miwili sasa.

Haki miliki ya picha AFP

Watu maelfu wameuwawa katika mashambulio ya chama hicho.

Kiongozi wa LRA, Joseph Kony anasakwa na Mahakama ya Jinai ya Kimaiatifa, ICC.

Akitangaza hatua hiyo, Rais Obama alisema maovu yaliyotendwa na LRA ni tishio kubwa kwa usalama wa eneo hilo.

Baada ya zaidi ya miongo miwili ya muaji, kunajisi wanawake, na ubakaji, alisema wakati umefika kukifyeka kikundi hicho.

Kikosi hicho cha Marekani kitayasaidia majeshi ya Uganda na nchi jirani katika kile kilichoelezewa kuwa kumuondoa kiongozi kiongozi wa LRA, Joseph Kony, vitani.

Kikosi hicho kitatumia vyombo vya teknolojia ya kisasa kabisa, kusaidia katika kile kinachoelezewa na wadadisi, kuwa sera ya ama kumkamata au kumuuwa Joseph Kony.

Lakini kikosi cha Marekani hakitashiriki katika mapambano ya vita, ila wakilazimika kujihami.

Kikosi hicho kimetumwa baada ya sheria kupitishwa karibuni Marekani, inayoruhusu kusaidia kuwapokonya silaha LRA, na kumfikisha kiongozi wake mbele ya mahakama.

Inavodhaniwa ni kuwa endapo Joseph Kony akikamatwa, basi na kikundi cha LRA kitasambaratika.