Shalit arudi Israel baada ya makubaliano

Haki miliki ya picha egyptian state tv
Image caption Gilad Shalit

Askari wa Israel Gilad Shalit amewasili Israel, kufuatia kuachiwa kwake baada ya kushikiliwa kwa miaka mitano ikiwa ni sehemu ya mpango wa makubaliano wa kubadilishana wafungwa na Hamas.

Sajini Shalit kwanza alichukuliwa ukanda wa Gaza na kupelekwa Misri, ambapo alikabidhiwa kwa maafisa wa Israeli na baadae kuvuka mipaka.

Zaidi ya Wapalestina 1,000 wanatarajiwa kuachiwa huru katika mpango wa kubadilishana wafungwa baina ya Israeli na Hamas.

Wafungwa wa mwanzo 477 wanaachiliwa huru siku ya Jumanne.

Sajini Shalit alitekwa mwaka 2006 na wapiganaji wa Hamas walioingia Israeli.

Mapema siku ya Jumanne Gilad Shalit, mwenye umri wa miaka 25, alipelekwa eneo la Rafah baina ya Gaza na Misri, na kukabidhiwa kwa Misri na Hamas, wakiwemo wawakilishi wa Israeli.

Televisheni ya Misri ilimwonyesha Sajini Shalit akisindikizwa kwa gari. Ni mara ya kwanza kuonekana kwenye video tangu mwaka 2009.

Baadae, katika mahojiano yake ya kwanza, aliiambia televisheni ya Misri kuwa anatamani kuiona familia yake na marafiki zake.

Akionekana kuwa dhaifu, alisema anatamani mabadilishano hayo ya wafungwa yasaidie kuleta amani baina ya Waisrael na Wapalestina.

Sajini Shalit baadae akapelekwa Kerem Shalom ambapo ni baina ya Misri na Israel.

Alipiga simu kwa wazazi wake kabla ya kusafirishwa kwenye kituo cha ndege cha Tel Nof.

Akifika huko atachunguzwa afya yake na kukutana na familia yake, pamoja na Bw Netanyahu.

Akionekana kuwa na afya njema, Sajini Shalit atapelekwa na familia yake kaskazini mwa Israeli na kusindikizwa na msafara nyumbani kwake Mitzpe Hila, magharibi mwa Galilee.

Wakati huo huo, takriban Wapalestina 180 miongoni mwa 295 wanaotarajiwa kupelekwa ukanda wa Gaza wamefika, ambapo sherehe zimeanza.