Prince Johnson amuunga mkono Sirleaf

Ellen Johnson Sirleaf Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Ellen Johnson Sirleaf

Aliyekuwa kiongozi wa waasi wa Liberia Prince Johnson, ambaye aliibuka wa tatu katika uchaguzi wa Liberia anasema anamuunga mkono mshindi wa tuzo ya amani ya Noble Ellen Johnson Sirleaf katika awamu ya pili.

"Yeye sio mbaya sana kati ya wawili hawa" aliiambia BBC. Vikosi vilivyotiifu kwa Bw. Johnson vilipigwa picha vikimtesa na kumuua mkandamizaji Samuel Doe.

Mpinzani wa Bi. Sirleaf atakuwa mwanabalozi wa zamani wa Umoja wa Mataifa Winston Tubman.

Huu ni uchaguzi wa pili wa Liberia tangu kumalizika vita ya wenyewe kwa wenyewe vya miaka 14 mwaka 2003.

Ikiwa kura karibu zote zimehesabiwa Bi. Sirleaf ana asilimia 44 dhidi ya 32 za Bw. Tubman ambapo Bw. Johnson ana asilimia 12.

Mgombe anahitaji zaidi ya asilimia 50 kupata ushindi wa moja kwa moja. Mwishoni mwa wiki, vyama vya upinzani ikiwa nipamoja vile vya Tubman na Johnson, vilisema vinajiondoa kutoka uchaguzi huo, vikiishutumu tume ya uchaguzi ya kitaifa kwa wizi wa kura kumsaidia Rais aliye madarakani.

Lakini Tubman amethibitisha kuwa atashiriki katika awamu ya pili ya uchaguzi huu ambao unatarajiwa kufanywa tarehe 8 mwezi November.

Bi. Sirleaf, ambaye mapema mwezi huu alikabidhiwa tuzo ya amani ya Nobel, alishinda uchaguzi wa mwaka 2005 na kuwa mwanamke wa kwanza Mwafrika kuchaguliwa kuwa Rais.

Alimshinda mcheza kandanda wa zamani George Weah, ambaye wakati huu ndiye mwenza wa Tubman katika uchaguzi huu.

Bi. Sirleaf bado hajasema lolote kuhusu hatua hiyo ya Johnson lakini kabla ya tangazo la Johnson alikuwa ameiambia BBC kuwa yuko tayari kufanya kazi na Waliberia wote.