Malaysia yawaokoa raia wa waganda

Image caption Wanawake wa Malaysia

Polisi nchini Malaysia wanasema wamesambaratisha mtandao unaofanya biashara ya kusafirisha watu ambao uliwalazimisha wanawake raia wa Uganda kwenye ukahaba.

Wanawake ishirini na mmoja wengi wao wakiwa na umri wa miaka 20, wameachiliwa huru katika msako mkali uliofanywa na polisi.

Walidanganywa kwa ahadi za kupata ajira zenye malipo makubwa kabla hawajapelekwa China na baadaye Malaysia walikoishia kuwa watumwa wa biashara ya ngono.

Wanawake hao wa Uganda walifichwa katika nyumba moja karibu na Kuala Lumpur.

Zaidi ya miezi mitatu iliyopita, wakalazimishwa kufanya ngono na wateja kwa saa kumi kwa siku.

Wanawake hao walipigwa na kubakwa na wateka nyara pindi walipojaribu kukataa. Muathirika mmoja alisimulia aliyoyapitia kwa afisa mmoja ubalozi wa Uganda ambaye alijifanya kuwa mteja.

Polisi wa Malyasia baadaye waliliweka jengo hilo chini ya linzi kwa wiki mbili kabla ya kulivamia ndani na kuwaokoa wanawake hao. Wanawake wenye biashara hiyo walikamatwa kwa kufanya biashara haramu ya watu.

Malaysia inatumika kwa yote kama mkondo wa kudafirishia na pia kituo cha wafanya biashara haramu ya watu.

Serikali mara kwa mara imekuwa ikikosolewa kwa udhibiti mdogo wa biashara hiyo na kuna tuhuma kwamba baadhi ya maafisa wa uhamiaji wanahusika na biashara hiyo.

Hii ndio sababu Marekani imeiweka Malaysia kwenye orodha ya nchi zinazofanya biashara hiyo katika miaka michache iliyopita.

Polisi wanasema hatua hii ya karibuni inaonyesha wako makini katika kulishughulikia tatizo hilo.