Mama mfaransa aliyetekwa Kenya afariki

Marie Dedieu Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Marie Dedieu

Maafisa wa Ufaransa wametangaza kuwa mama raia wa kifaransa aliyetekwa nyara kutoka Kenya na watu wanaoshukiwa kuwa wanamgambo wa Kisomali mapema mwezi huu amefariki.

Maafisa wa kibalozi wanasema walifahamishwa kifo cha Marie Dedieu na watu ambao wamekuwa wakijaribu kuzungumza na watekaji nyara ili wamuachie huru mama huyo.

Wamesema kuwa hawajui alikufa lini na nini kilichosababisha kifo chake, ingawa inakumbukwa kuwa afya yake ilikuwa dhaifu na kuwa hakuruhusiwa kutumia dawa, tukio kama hili lilitarajiwa.

Bi. Dedieu mwenye umri wa miaka 66 ni mmoja wa wageni kutoka mataifa ya magharibi waliotekwa kutoka Kenya mwezi October.

Mwezi September raia kutoka Uingereza David Tebbutt aliuawa na mke wake Judith kutekwa katika hoteli moja ya kifahari huko Kiwayu pwani ya Kenya.

Na mwezi jana wanawake wawili raia wa Uhispania wafanyakazi wa misaada walitekwa kutoka kambi ya wakimbizi ya Dadaab karibu na mpaka wa Kenya na Somalia.

Wanawake wote watatu waliotekwa bado hawajulikani walipo.

Bi.Dedieu ambaye alitumia kiti cha magurudumu na dawa kila mara kutokana na matatizo ya moyo na vile vile saratani, alikuwa akiishi Kenya tangu miaka ya 90.

Alitekwa nyara kutoka nyumbani kwake katika kisiwa kidogo cha Manda katika eneo la Lamu tarehe moja mwezi October na watu waliokuwa na silaha.

Maafisa wamethibitisha alisafirishwa kwa boti hadi Somalia na kuwa waliomteka nyara hawakuchukuwa kiti chake cha magurudumu ama dawa zake wakati wakimteka.

Wizara ya mashauri ya kigeni ya Ufaransa imesema inawataka waliohusika wote wafikishwe mbele ya vyombo vya sheria.

Wanaoshutumiwa kwa utekaji huu ni kundi la wanamgambo wa kiislamu la al-Shabab ambao wanadhibiti eneo kubwa la kusini na Somalia ya Kati.

Somalia imekabiliwa na mapigano ya mwenyewe kwa wenyewe kwa miongo miwili, hili limesababisha silaha kupatikana kwa urahisi na kuna makundi mengi ya watu wenyewe silaha ambao pia wanaweza kuwa walihusika na utekaji huo.

Waandishi wanasema al-Shabab hawajawahi kuwateka wageni nje ya eneo lao ilhali magenge ya maharamia huendesha shughuli zao nje ya Somalia, kawaida huteka meli na wafanyakazi wake na kuitisha pesa, magenge haya hayafanyi shughuli zake nchi kavu.

Kenya kwa upande wake imejibiza msururu huu wa utekaji nyara kwa kupeleka majeshi hadi Somalia kukabiliana na wanamgambo.

Hatahivyo, kumekuwa na taarifa za kutatanisha kutoka Kenya na serikali ya mpito ya Somalia kuhusu kuwepo kwa vikosi vya Kenya nchini Somalia.

Al-Shabab wamekanusha kuhusika na utekaji nyara wowote na wameonya kuishambulia Kenya ikiwa wanajeshi wake hawataondoka.