Kenya kuanzisha harakati za kiusalama

Majeshi ya Kenya Haki miliki ya picha AFP
Image caption Majeshi ya Kenya

Kenya inapanga kuanzisha harakati za kiusalama ndani ya nchi dhidi ya washirika wa kundi la wapiganaji wa Al Shabaab.

Kulingana na naibu waziri wa mambo ya ndani wa serikali ya Kenya, Orwa Ojodeh, harakati hizo zitakuwa kubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa na zitafanyika mjini Nairobi.

Maeneo yatakayolegwa ni kama vile mtaa wa Eastleigh ulioko Mashariki mwa mji huo, ambako raia wengi kutoka Somalia wanaishi.

Akitangaza mpango huo bungeni, Bw Ojodeh ameelezea vita dhidi ya al shabaab kama '' mnyama mkubwa ambao mkia wake uko ndani ya nchi ya Somalia na kichwa cha mnyama huyo kimejikita katika mtaa wa Eastleigh''.

Mtaa wa Eastleigh una idadi kubwa ya raia wa Kenya wenye asili ya Kisomali na wale kutoka Somalia .

Hata hivyo tangazo hilo halijapokewa vyema na baadhi wa wabunge.

Katika mikakati hiyo ya kiusalama ambayo bado haijulikana ni lini itaanza , wanaotumia usafiri wa angani na ardhini watakaguliwa watakopokua wakielekea na kutoka katika maeneo yanayopakana na nchi ya Somalia.

Tangu harakati za kijeshi za kuwasaka al shabaab kwa jina "operesheni linda nchi" zianze siku tano zilizopita, ulinzi umeimarishwa katika maeneo muhimu kama vile vituo vya usafiri, mahoteli, maeneo yanayotembelewa na watalii na maduka makubwa.

Hata hivyo wadadisi wa masuala ya usalama wanasema, mikakati inayopangwa kufanyika mjini Nairobi haitakuwa rahisi, kwani ni vigumu kutofautisha Wasomali kutoka Kenya na wale wa Somalia.

Pia, wengi wa raia wa Kisomali walioingia Kenya, waliweza kupata vitambulisho vya Kenya kwa kupitia njia za magendo.