ICC yailaumu Malawi kutomkamata Bashir

Rais  Omar al Bashir Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Rais Omar al Bashir

Mahakama ya kimataifa ya ICC imeitaka Malawi kueleza kwanini ilikosa kumkamata Rais wa Sudan Omar al-Bashir alipoizuru nchi hiyo hivi majuzi.

Mahakama hiyo tayari imeshatoa hati ya kumkamata Bw Bashir kutokana na mashtaka ya mauwaji ya halaiki na uhalifu wa kivita katika mzozo wa Darfur.

Malawi imetia saini mkataba ulioidhinisha kuanzishwa kwa mahakama hiyo ya kimataifa ya uhalifu wa kivita lakini imesema sio jukumu lake kumkamata BW Bashir.

Rais Bashir anakanusha madai dhidi yake akisema yamechochewa kisiasa.

Muungano wa Afrika umekuwa ukifanya juhudi agizo la kumkamata lisitishwe na kuishutumu mahakama hiyo kwa kuchunguza madai ya uhalifu wa kivita Afrika tu na kusema kuwa kumkamata Rais Bashir kutatatiza juhudi za kuleta amani Darfur.

Bw Bashir alikaribishwa kwa gwaride la heshima alipowasili katika mji mkuu wa Malawi, Lilongwe kuhudhuria kikao cha biashara mwishoni mwa wiki.

Muungano wa Ulaya na makundi ya haki za binadamu yaliitaka Malawi imkamate Bashir.

Lakini Waziri wa habari wa Malawi Patricia Kaliati ameiambia BBC kuwa Malawi haingeweza kumkamata Rais Bashir kwa kuwa alikuwa anahudhuria kikao cha viongozi wa jumuiya ya biashara ya nchi za kusini na mashariki mwa Afrika-COMESA.

"Amekuwa kwa shughuli za kibiashara na hatuna sababu za kumkamata Rais Bashir" aliongeza Waziri wa habari wa Malawi.

Kenya na Chad,ikiwa pia nazo zilitia saini kuanzishwa mahakama hiyo, pia zilimruhusu Rais Bashir kuzitembelea.

Rais Bingu wa Mutharika wa Malawi ni mmoja wa viongozi kadhaa wa Afrika kuishutumu mahakama hiyo kuwa inachunguza madai ya uhalifu wa kivita Afrika tu na sio kwengineko.

Bw Bashir ndio kiongozi wa kwanza kushtakiwa na mahakama ya ICC ambao inamshtaki kwa mauaji ya halaiki na uhalifu wa kivita Darfur.

Watu milioni 2.7 wamekimbia makwao tangu mzozo kuanza Darfur mwaka 2003 na Umoja wa Mataifa unasema karibu watu 300,000 wamekufa, wengi wao kutokana na magonjwa.

Serikali ya Sudan inasema mzozo huo umesababisha vifo vya watu 12,000 na kuwa idadi inayotolewa imeongezwa kutokana na sababu za kisiasa.