Uchaguzi huru wafanywa Tunisia

Wananchi wa Tunisia wanapiga kura leo kuchagua bunge litalotayarisha katiba mpya na kumteua rais wa muda.

Haki miliki ya picha Reuters

Tunisia ilikuwa ya mwanzo kuanza ghasia za mabadiliko katika nchi za Kiarabu baada ya kijana mmoja, Mohamed Bouazizi kujichoma moto, kupinga dhuluma za uongozi.

Huu ndio uchaguzi wa mwanzo huru tangu Tunisia kupata uhuru kutoka kwa Ufaransa mwaka wa 1956, na uchaguzi wa mwanzo tangu maandamano ya mabadiliko kuanza katika nchi za Kiarabu.

Watunisia wanafanya uchaguzi haraka, miezi 10 tu baada ya dikteta Zine al-Abidine Ben Ali kuondoshwa.

Vyama zaidi ya mia moja vinashiriki, kimojawapo ni cha Kiislamu, ambacho kilipigwa marufuku na Ben Ali, na ndicho kilichojitayarisha vema.

Kinatarajiwa kupata kura nyingi kushinda chama chochote kile.

Kampeni kwenye internet inakiponda chama hicho kuwa kina msimamo mkali, lakini viongozi wake wanasema wanapinga utawala wa Kiislamu na wanataka uwazi, uvumilivu, na nchi kutokuwa na chama kimoja kitachogubika vengine.

Vyama visivokuwa vya Kiislamu piya vinatarajiwa kufanya uzuri.

Kampeni zao zilihusu maswala ya kiuchumi, kijamii, biashara za kibinafsi, ajira na usawa.

Watu ndani ya nchi na katika nchi za Kiarabu wanataraji mengi kutoka Tunisia, kwa sababu Tunisia ndio iliyoanzisha maandamano ya mabadiliko.

Na wananchi wenyewe wana hamu kuwa nchi yao ifanikiwe.