Wafuasi wa Gaddafi 'waliuawa'

Haki miliki ya picha
Image caption Libya

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch HRW limesema mauaji makubwa ya watu 53 wanaomwuunga mkono marehemu Kanali Gaddafi yalionekana kufanyika mjini Sirte, kwenye ngome yake ya mwisho.

Shirika hilo limesema katika ripoti yao iliyotolewa leo kuwa miili ya watu waliyooza, baadhi wakiwa wamefungwa mikono kwa nyuma walikutwa kwenye hoteli iliyotelekezwa ya Mahari.

Hoteli hiyo ilikuwa kwenye eneo lililokuwa limedhibitiwa na majeshi yanayompinga Kanali Gaddafi kabla ya mauaji kutokea.

HRW limesema miili hiyo ilikuwa imekusanyika sehemu moja inayoelekea kuwa ndipo walipouawa katika bustani ya hoteli moja iliyo ufukweni mwa bahari.

Baadhi yao walikuwa wamefungwa mikono yao nyuma kwa nyuzi za plastiki.

Kulikuwa na matundu ya risasi ardhini na matone ya damu iliyokuwa inatiririka chini ya miili hiyo.

Ushahidi unaonyesha kwamba takriban wote waliuawa kwa kupigwa risasi wakati wakizuiliwa katika hoteli hiyo.

Majina ya vikundi kadhaa vya wapiganaji wapinzani wa hayati Kanali Gaddafi yaliandikwa juu ya kuta ya hoteli hiyo iliyotelekezwa, ikimaanisha vikundi hivyo vilikua vinadhibiti eneo hilo.

Wenyeji wa eneo hilo wameviambia vikundi vya kutetea haki za binaadamu kuwa wengi wa waathiriwa walikuwa ni wakaazi wa Sirte.

Miongoni mwao wakiwemo maafisa wa zamani wa serikali ya Kanali Gaddafi na afisa wa kijeshi.

Human Rights Watch imelihimiza baraza la mpito la taifa ambalo sasa limekwishatangaza kuikomboa nchi nzima, ifanye uchunguzi wa haraka na ulio wazi kuhusu mauaji hayo ya jumla na kuwafikisha mahakamani wote waliohusika.

Shirika hilo limesema inaelekea kile ilichokieleza kuwa "mauaji haya mapya"ni sehemu ya vitendo vya kawaida vya mauaji na ukiukwaji wa haki za binadamu vya wapiganaji wanaompinga Gaddafi ambao wanajichukulia kuwa wako juu ya sheria.