Kura zahesabiwa katika uchaguzi wa kihistoria Tunisia

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Tunisia: Uchaguzi wa kihistoria

Maafisa wa tume ya uchaguzi nchini Tunisia wanaendelea kuhesabu kura baada ya uchaguzi wa Jumapili, ikiwa ni wa kwanza huru tangu kutokea kwa mapinduzi ya kiraia katika nchi za kiarabu.

Zaidi ya 90% ya wale waliosajiliwa kupiga kura walijitokeza kushiriki kwenye mchakato huo, maafisa wamesema.

Raia wa Tunisia wanachagua wajumbe 217 ambao wataandika katiba na kuteua serikali ya muda.

Marekani na muungao wa Ulaya wamepongeza Tunisia kwa uchaguzi wa amani, huku Rais Barack Obama akisema kuwa uchaguzi huo ni "hatua muhimu sana".

Rais wa zamani Zine al-Abidine Ben Ali aliondolewa madarakani miezi tisa iliopita kufuatia maandamano - alikuwa madarakani kwa muda wa miaka 23.

Katibu mkuu wa tume ya uchaguzi Boubaker Bethabet anasema zaidi ya asilimia 90% ya watu milioni 4.1 waliosajiliwa walipiga kura.