Jaji Mkuu Tanzania awania nafasi ya Ocampo

Haki miliki ya picha ipp media
Image caption Jaji Mkuu wa Tanzania Mohamed Chande Othman kuwania nafasi ya Ocampo ICC

Jaji mkuu wa Tanzania Mohamed Chande Othman ni mmoja kati ya watu wanne muhimu wanaoweza kushika nafasi ya Mwendesha Mashtaka katika Mahakama ya Uhalifu ya Kimataifa iliyoko The Hague, nchini Uholanzi.

Nafasi hiyo ambayo kwa sasa inashikiliwa na Luis Moreno-Ocampo itakuwa wazi hapo mwakani baada ya Bw Ocampo kumaliza kipindi chake cha utumishi wa miaka tisa mwakani.

Kwa mujibu wa shirika la habari la AF, wagombea wengine ni pamoja na Naibu Mwendesha Mashtaka wa sasa Fatou Bensouda wa Gambia, ambaye wengi wanamwona kuwa analeta ushindani mkali.

Anaungwa mkono na Umoja wa Afrika ambao mara nyingi umemkosoa Moreno-Ocampo kwa kufungua uchunguzi wa mataifa ya Afrika pekee.

Katika orodha hiyo pia yupo Andrew Cayley, mwendesha mashtaka mwenza katika mahakama maalum ya Khmer Rouge nchini Cambodia anayetokea Uingereza.

Mwingine ni Robert Petit, ambaye ni mshauri kuhusu uhalifu dhidi ya ubinadamu na uhalifu wa kivita katika Kitengo cha Mahakama nchini Canada.

Kamati ya iliyoundwa na nchi wanachama wa mahakama hayo awali ilikuwa na orodha ya majina 52 ya wagombea walioomba kupendekezwa katika nafasi hiyo ya juu. Kamati hiyo iliwahoji wanane kabla ya kupata wagombea wanne.

Kwa mujibu wa Kamati hiyo ‘

Wote wana uzoefu mkubwa katika kuendesha kesi za kimataifa.

Jaji Othman ameshika nafasi muhimu mbalimbali za uandamizi katika mfumo wa sheria nchini Tanzania na alikuwa mwendesha mashtaka mkuu katika mahakama maalum ya mauaji ya Rwanda na pia mwendesha mashtaka katika Utawala wa Mpito wa Umoja wa Mataifa katika Timor Mashariki.

Kabla ya kujiunga na mahakama maalum ya Khmer Rouge , Bw Cayley alikuwa mwendesha mashataka mshauri mwandamizi wa ICC, Wakili wa Utetezi katika mahakama maalum za vita vya Sierra Leone na Yugoslavia na pia mwendehsa mashtaka katika mahakama ya Yugoslavia.

Petit alikuwa wakili mwandamizi katika kesi kwenye Mahakama ya Sierra Leone, afisa wa sheria katika mahakama maalum ya Rwanda na mshauri wa sheria kwa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Kosovo.

Bensouda ni waziri wa zamani wa sheria nchini Gambia ambaye pia aliwahi kufanya kazi kama mshauri mwandamizi wa sheria na wakili katika kesi kwenye Mahakama maalum ya Rwanda.

"Ni orodha nzito kabisa," Alisema Param-Preet Singh, Mshauri Mwandamizi katika kitengo kinachoshughulikia Haki za Binadamu cha Human Rights Watch's International Justice Program.