Syria 'inatesa wagonjwa hospitali' -Amnesty

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Maandamano nchini Syria

Wagonjwa katika hospitali za uma nchini Syria wanateswa kama njia moja ya kukandamiza upinzani, imedaiwa katika ripoti iliyotolewa na shirika la kutetea haki za binaadamu la Amnesty International.

Katika ripoti hiyo ya kurasa 39 inadaiwa kuwa wagonjwa katika karibu hospitali nne za uma wamekuwa wakiteswa na kufanyiwa vitendo vingine vibaya, maafisa wengine wa afya wakitajwa kuhusika katika mambo hayo.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo wengi ya raia waliojeruhiwa wanaona ni salama kwao kutokwenda hospitali.

Serikali ya Syria imekanusha kuwatesa wapinzani wa serikali.

Maandamano dhidi ya serikali, ambayo yalianza mwezi wa tatu, yameendelea licha ya hatua ya Rais Bashar al-Assad kujaribu kuzima maandamano hayo.

Umoja wa Mataifa unasema kuwa zaidi ya watu 3,000 wamefariki dunia katika muda wa miezi saba ya maandamano, ambayo serikali ya Syria imesema yanaongozwa na "magaidi" na "makundi yenye silaha".

Waandishi wa habari wa kimataifa hawaruhusiwi nchini Syria, na ni vigumu kuthibitisha taarifa hizo.