Chama cha kiislamu chajitangazia ushindi Tunisia

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Uchaguzi wa kihistoria

Chama cha kiislamu chenye msimamo wa wastani nchini Tunisia, Ennahda, kimejitangazia ushindi katika uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia nchini humo.

Matokeo rasmi yanatarajiwa baadaye siku ya Jumanne, lakini matokeo ya awali yanaonyesha kuwa chama cha Ennahda kitapata kura nyingi zaidi.

Wapinzani wao wakuu, chama kinachofuata mfumo usio wa kidini cha PDP, wamekubali kushindwa.

Waangalizi wa uchaguzi wa kimataifa wameupongeza uchaguzi huo wa Jumapili na kuutaja kuwa wa huru na haki.

Aliyekuwa Rais wa Tunisia Zine al-Abidine Ben Ali aliondolewa madarakani miezi tisa iliopita baada ya maandamano ya raia - amekuwa madarakani kwa muda wa miaka 23.

Hata hivyo, tofauti na majirani zao wa upande wa mashariki Libya, mchakato wa mabadiliko ya uongozi nchini Tunisia kutoka kwa utawala wa dikteta umekuwa wa amani.

Viongozi wa Ennahda wameahidi kuwa na mfumo wa vyama vingi, demokrasia isiyo ya mfumo wa kidini, na taifa lisilo la kiislamu.

Msemaji wa chama hicho, Yusra Ghannouchi, amesema: "raia wa Tunisia wamepigia kura vyama ambavyo vimekuwa katika harakati za kupigania demokrasia na kupinga utawala wa kidikteta wa Ben Ali.