Kenya:Polisi wanasa maguruneti na bunduki

Haki miliki ya picha internet
Image caption Usalama umeimarishwa

Mtu mmoja amekamatwa na polisi na silaha mbali mbali kunaswa katika mtaa mmoja mjini Nairobi,Kenya.

Katika nyumba hiyo polisi walinasa maguruneti 13 na bunduki kadhaa pamoja na risasi.

Kwa mujibu wa mkuu wa polisi nchini Kenya Mathew Iteere, mtu aliyekamatwa anashukiwa kuwa mwanachama wa kundi la kigaidi.

"Sina shaka kuwa tutapata habari muhimu kutoka kwake na kuweza kuwatia mbaroni wanachama wengine wa makundi ya kigaidi," alisema.

Majirani wanasema mtu huyo alihamia katika nyumba hiyo ya kupanga kama mwezi mmoja uliopita na kwamba hawajawahi kumuona mtu mwingine yeyote hapo.

Polisi wanasema walivamia nyumba hiyo kutokana na taarifa za kijasusi walizopata.

Hatua hiyo inakuja baada ya mashambulio mawili kutokea katika maeneo tofauti mjini Nairobi.Katika mashambulio hayo mtu mmoja alifariki dunia na wengine zaidi ishirini kujeruhiwa.