Tunisia yataka kumkamata mjane wa Arafat

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Suha Arafat

Serikali ya Tunisia imetoa hati ya kimataifa ya kukamtwa kwa Suha Arafat, mjane wa aliyekuwa kiongozi wa Palestina Yasser Arafat.

Wizara ya sheria ilisema anashukiwa kwa kujihusiha na ufisadi akishirikiana na familia ya rais aliyeondolewa Zine al-Abidine Ben Ali.

Bi Arafat alikuwa muda mwingi nchini humo na kuanza biashara na mke wa Ben Ali, Leila Trabelsi.

Shirika la habari la AFP limesema, amekana mashtaka hayo.

Familia za Ben Ali na Trablesi zilidhibiti sehemu kubwa ya uchumi wa Tunisia.

Baada ya kifo cha Bw Arafat mwaka 2004, Bi Arafat alipewa uraia wa Tunisia na kuanzisha shule ya kimataifa kwenye mji wa Carthage na Trabelsi.

Uhusiano baina ya wawili hao ulivurugika na mwaka 2007 alinyang'anywa uraia huo na kulazimishwa kuondoka nchini humo.

Aliyekuwa rais Ben Ali alipinduliwa mwezi Januari, katika harakati maarufu za kutaka mabadiliko kwenye nchi za kiarabu, na kukimbilia Saudi Arabia.

Serikali ya mpito ya Tunisia imefungua kesi dhidi ya watu chungu nzima wanaoshukiwa kujihusisha na ufisadi wakati wa uongozi wa Ben Ali uliodumu kwa miaka 23.

Mahakama za Tunisa zimemtia hatiani Ben Ali na Trabelsi bila wao kuwepo mahakamni kwa makosa ya wizi, ufisadi na mashtaka mengine, ambapo zote wamezikana.

Uhusiano wa Arafat na Tunisia umeanza miaka ya 80 baada ya Palestinian Liberation Organisation ulipoanzisha makao yake makuu mjini Tunis.

Inaripotiwa kuwa Bi Arafat anaishi Malta.