Tunisia: Chama cha Ennahda chaelekea kupata ushindi

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Wafuasi wa Ennahda

Matokeo yaliyotangazwa kufikia sasa Tunisia yanaashiria ushindi kwa chama cha kiislamu chenye msimamo wa wastani Ennahda, katika uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia uliotokana na mapinduzi ya kiraia kwenye nchi za kiarabu.

Tume ya uchaguzi imesema chama cha Ennahda kimepata kura nyingi zaidi katika uchaguzi wa bunge jipya ambalo litaongoza mchakato wa kuandika katiba mpya na kuchagua serikali ya muda.

Hata hivyo Ennahda haitarajiwi kupata idadi kubwa ya wajumbe itakayowapa uwezo wa kubuni serikali. Mazungumzo ya muungano na vyama visivyoegemea upande wowote wa dini yameanza.

Uchaguzi huo wa Jumapili umepongezwa na wachunguzi wa uchaguzi.

Ulikuwa ni uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia nchini Tunisia, tangu kuondolewa madarakani aliyekuwa Rais Zine al-Abidine Ben Ali, mwezi Januari kufuatia maandamano. Amekuwa madarakani kwa muda wa miaka 23.

Hata hivyo,tofauti na jirani zake wa upande mashariki Libya, mageuzi nchini Tunisia kutoka kwa utawala wa kidikteta kwa sehemu kubwa yamekuwa ya amani.

Siku ya Jumanne tume ya uchaguzi ilisema kuwa Ennahda imeshinda viti 15 kati ya 39 ambavyo matokeo yake yametolewa kufikia sasa vilivyotangazwa katika bunge jipya la wajumbe 217.