Qantas yavunja safari za ndege

Shirika la Ndege la Australia la Qantas limesimamisha safari za ndege zake zote, kwa sababu ya mzozo wa muda mrefu na vyama vya wafanyakazi.

Haki miliki ya picha Reuters

Qantas ilisema safari zote za ndani ya nchi na za kimataifa, zimevunjwa.

Ilisema kuwa watumishi wote hawataruhusiwa kuingia makazini hadi vyama vya wafanyakazi vikubali kufikia makubaliano na viongozi wa kampuni.

Zaidi ya ndege 100 zimevunja safari katika viwanja vya ndege 22, katika sehemu mbalimbali za dunia.

Maelfu ya abiria wameathirika.

Mkuu wa kampuni, Alan Joyce, alisema ilibidi kuchukua hatua hiyo, kwa sababu vyama vya wafanyakazi vinaidharau kampuni.

Wafanyakazi wa Qantas wamegoma mara kadha kwa sababu ya mishahara na mipango ya kampuni ya kuhamisha kazi kadha na kuzipeleka nchi za nje.

Waziri Mkuu wa Australia, Julia Gillard, ameonya kuwa mzozo huo unaweza kuumiza uchumi wa nchi.

Na shirika la ndege la Ufaransa, Air France, nalo linasema limefuta asili-mia-ishirini ya safari zake, kwa sababu ya mgomo wa watumishi wa ndani ya ndege.

Waziri wa usafiri wa Ufaransa, Thierry Mariani, alisema wafanyakazi hao wanajivunjia riziki wenyewe.