Kenya yakanusha kuua raia Somalia

Haki miliki ya picha internet
Image caption Ndege zililenga kambi ya Al Shabaab

Raia 10 waripotiwa kuuawa na wengine 50 kujeruhiwa baada ya ndege za kivita za Kenya kuwashambulia wapiganaji wa al-shabaab kusini mwa Somalia.

Msemaji wa Jeshi la Kenya ameiambia BBC kuwa ndege hizo zilishambulia maeneo yaliyo viungani mwa mji wa Jilib.

Amesema waliouawa ni wapiganaji wa kundi hilo lililo na ushirikiano na mtandao wa Al-qaeda.

Lakini shirika la madaktari wasio na mipaka la Medecins Sans Frontieres (MSF) limesema kwa sasa linawatibu watu waliojeruhiwa baada ya kambi ya wakimbizi kushambuliwa na kusababisha vifo vya watu watatu.

Majeshi ya Kenya yaliingia hadi Somalia ili kukabiliana na wapiganaji wa al-shabaab.

Nchi hiyo ya Afrika Mashariki inawalaumu wapiganaji wa al shabaab kwa kuvuka mpaka sehemu za Kaskazini Mashariki na kushambulia vikosi vya Kenya na pia kwa visa kadhaa vya utekaji nyara.

"Tulipokea taarifa za kijasusi kuwa kiongozi mmoja wa al-shabaab alikuwa amepanga kuzuru kambi ya Jilib na ndipo tukafanya mashabulio kutoka angani " msemaji wa jeshi la nchi kavu la Kenya Meja Emmanuel Chirchir ameiambia BBC.

" Taarifa tulizo nazo ni kuwa wapiganaji 10 wa al-shabaab wameuawa na wengine 47 kujeruhiwa", aliongezea kusema.

Amekanusha habari kuwa kambi ya raia ilishambuliwa akisema taarifa kuwa kambi ya wakimbizi ilishambuliwa na raia wa kawaida kuuawa ni propaganda za al-shabaab.

Hata hivyo katika taarifa yake ya Jumapili ,shirika la MSF limesema kuwa wahudumu katika hospitali iliyoko Marere inawahudumia watu kadhaa waliojeruhiwa kufuatia shambulio la angani katika mji wa Jilib.

Shirika hilo limesema kuwa kambi ya wakimbizi wa ndani kwa ndani ilishambuliwa majira ya saa saba na nusu mchana, saa za Afrika mashariki na waliopokelewa ili watibiwe wengi wao ni wanawake na watoto.

Kundi hilo la al-Shabaab limekanusha kuwa linahusika na visa vya utekaji nyara nchini Kenya na linataka Kenya iondowe wanajeshi wake au wakabiliwe vikali.