Mwalimu apigwa hadi kufa Afrika kusini

Haki miliki ya picha the star
Image caption Mkuu wa shule Noko Moabelo

Raia mmoja wa Afrika kusini ameshtakiwa kwa mauaji baada ya kaka yake kupigwa hadi kufa mbele ya wanafunzi wake karibu na mji wa Polokwane kaskazini mwa nchi hiyo.

Guilford Shapo, mwalimu katika shule ya msingi ya Masehlong, alishambuliwa alipokuwa akisimamia mitihani siku ya Jumanne, chombo cha habari cha umma cha Afrika kusini kiliripoti.

Mdogo wake wa kiume Happy Shapo ameshtakiwa kwa uhalifu huo, msemaji wa polisi Ronel Otto aliiambia BBC.

Bw Shapo hakutakiwa kusema lolote na kesi hiyo imeahirishwa hadi wiki ijayo.

Gazeti la nchi hiyo la Star lilimnukuu Noko Moabelo, mkuu wa shule katika kijiji cha Ga-Mmasehlong kwenye jimbo la Limpopo akisema, " Tulishtushwa na wanafunzi walipopiga kelele na kukimbia kutoka darasani."

Alisema, "Bw Shapo alikuwa mwalimu pekee wa kiume katika shule hiyo. Tukiwa wanawake, hakuna hata mmoja wetu ambaye angeweza kujaribu kupambana na mshukiwa huyo."

Majirani waliosikia makelele hayo walikimbilia shuleni hapo kusimamisha mashambulio hayo ya mapanga, gazeti hili liliripoti.

Guilford Shapo alifariki dunia baadae kutokana na majeraha.

Luteni Kanali Otto alisema ombi lake la dhamana litasikilizwa Novemba 21 siku ya Jumatatu.

Idadi ya matukio ya mauaji yamepungua sana Afrika kusini tangu kumalizika kwa enzi za ubaguzi wa rangi mwaka 1994, lakini bado matukio hayo yanaongoza ukilinganisha na nchi nyingine baada ya kutokea zaidi ya mauaji ya watu 40 kwa siku.