Congo yakerwa na vitisho vya upinzani

Haki miliki ya picha VT Freeze Frame
Image caption Bw Etienne Tshisekedi

Vitisho vilivyotolewa na kiongozi wa upinzani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Etienne Tshisekedi vinaweza kuchukuliwa kuwa uhaini, serikali imesema.

Bw Tshisekedi amesema anajichukulia kama rais na kuzitaka mamlaka husika kuwaachia huru wafuasi wake waliokamatwa wakati wa maandamano ya hivi karibuni.

Amewasihi watu kutoroka jela kama hawajaachiliwa huru mpaka ifikapo siku ya Jumanne.

Makundi ya kutetea haki za binadamu yameonya kwa usalama kuporomoka huku uchaguzi mkuu wa Novemba 28 ukikaribia.

Ni uchaguzi wa pili tangu kumalizika kwa mapigano yenye ukatili mkubwa yaliyodumu kwa miaka mitano iliyoenea mpaka nchi jirani.

Bw Tshisekedi aligomea uchaguzi mwaka 2006, akisema kulifanyika hila.

Makataa

Wakati wa mahojiano ya moja kwa moja ya simu kupitia kituo cha televisheni cha upinzani cha RLTV Jumapili jioni, Bw Tshisekedi, mwenye umri wa miaka 78, alisema kwa wakati uliobaki wa mchakato wa uchaguzi mamlaka husika ziripoti kwake kwani "watu wengi wananiunga mkono mimi".

Siku ya Jumatatu, chama cha Bw Tshisekedi cha Union for Democracy and Social Progress (UDPS) kilithibitisha kuwa kiongozi wao ndiye aliyefanyiwa mahojiano.

Alizungumza kwa lugha ya Kilingala magharibi mwa Congo ambapo ndipo anaungwa mkono zaidi.

Maafisa wa UDPS waliiambia BBC wako tayari kuandamana mpaka gereza kuu kwenye mji mkuu, Kinshasa, siku ya Jumanne.

Kutokana na hilo, waziri wa habari wa Congo Lambert Mende aliifunga RLTV huku kukifanywa uchunguzi na wadhibiti wa vyombo vya habari, tume ya uchaguzi na mahakama.

Bw Mende alisema, "tuna wasiwasi sana na afya ya akili ya akili ya kiongozi wa UDPS."