Tanzania yawakamata askari wa Congo

Image caption Tanzania

Zaidi ya askari 20 wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wametiwa kizuizini nchini Tanzania kwa kuingia kaskazini -magharibi mwa nchi hiyo kinyume cha sheria, jeshi la Tanzania limesema.

Walisema walikuwa wakiwafuata waasi kutoka Congo wanaopata matibabu Tanzania, alisema Lt Kanali Emmanuel Mcheri.

Watu hao wenye silaha kali walikamatwa baada ya kutia nanga karibu na boti ya polisi katika bandari ya Kigoma kwenye ziwa Tanganyika.

Eneo la mashariki mwa Congo lenye utajiri mkubwa wa madini limegubikwa na makundi ya waasi.

Lt Kanali Mcheri alisema askari hao, ambao bado wanahojiwa, walikuwa na bunduki, maguruneti, bastola na risasi nyingi.

Aliiambia BBC Swahili, " Wamevunja usalama wa nchi yetu kwa kuingia nchini kwetu na silaha nzito. Nimeshatoa taarifa kwa viongozi waandamizi serikalini na nasubiri maagizo zaidi."

Maafisa wa eneo hilo wamekataa kuzungumzia suala hilo.

Licha ya kuwepo makubaliano ya amani huko Congo mwaka 2002, uliomaliza mapigano mabaya ya wenyewe kwa wenyewe yaliyodumu kwa miaka mitano, bado kuna vurugu mashariki mwa nchi hiyo.

Majeshi ya kutunza amani ya umoja wa mataifa yamekuwa yakiunga mkono juhudi za kupambana na baadhi ya wapiganaji mashariki mwa Congo na kuwahusisha wengine kwenye jeshi la nchi hiyo.

Takriban wakimbizi 42,000 wa Congo wako Tanzania, wakiwa wamekimbia mapigano mashariki mwa Congo, kulingana na shirika linalowatunza wakimbizi la umoja wa mataifa.