Wasiwasi kuhusu kuenea kwa silaha Libya

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeelezea "wasiwasi wake" juu ya suala la kuenea kwa silaha nyingi nchini Libya zilizonunuliwa wakati wa utawala wa Kanali Muammar Gaddafi.

Baraza hilo limetoa wito kwa Libya na majirani wake kuhakikisha kuwa silaha hizo ambazo zimeibwa zimeondolewa.

Kumekuwa na wasiwasi kuwa silaha hizo huenda zikaingia mikononi mwa al-Qaeda na makundi mengine ya wapiganaji.

Silaha nyingi ziliangamizwa wakati wa harakati za Nato, ambazo zilimalizika usiku wa Jumatatu.

Hata hivyo, maafisa wamesema kuwa haifahamiki ni kiasi gani cha silaha ambacho bado kipo nje.

Mswada, ulioandikwa na Urusi na kuidhinishwa na wajumbe wote, unasema kuwa idadi kubwa ya makombora yanayorushwa kutoka usawa wa bega, yaliyonunuliwa wakati wa utawala wa Kanali Gaddafi, huenda ikaleta hatari ya udunguaji wa ndege.

Unasisitiza kuwa "kuenea kwa silaha zote... hasa, makombora yanayoweza kubebwa na watu, katika kanda hiyo, kunaweza kukasababisha kukithiri kwa vitendo vya kigaidi, ikiwemo vile vya al-Qaida katika eneo la kaskazini mwa Afrika".

Mswada huo pia ulitoa wito kwa serikali mpya ya Libya kuziangamiza silaha za sumu kwa kushirikiana na mamlaka za kimataifa.