Mutai aweka rekodi mpya New York

Mutai Haki miliki ya picha online
Image caption Mutai avunja rekodi isiyo rasmi

Geoffrey Mutai wa Kenya ameshinda mbio za New York Marathon na kuweka rekodi mpya ya mbio hizo.

Mutai amemaliza katika muda usio rasmi wa saa mbili, dakika tano na sekunde sita,- zaidi ya dakika mbili ya muda wa zamani.

Mkimbiaji huyo mwenye umri wa miaka 30, sasa amejiweka katika wakimbiaji ambao wanadhaniwa watan'gara katika michuano ya Olimpiki ya mwakani, baada ya kuweka rekodi ya pili mwaka huu.

Mwezi Aprili, Mutai alikimbia kwa kasi ya kihistoria katika mbio za Boston: 2:03:02.

Hata hivyo muda huo haukutajwa kama rekodi ya dunia kwa sababu njia ya mbio hizo inadhaniwa kuwa imenyooka sana na ina mteremko mkali.

muda wa wakimbiaji katika nafasi ya pili na ya tatu ulikuwa ndani ya rekodi ya zamani ya mbio za New York ya 2:07:43 iliyowekwa na Tesfaye Jifar wa Ethiopia miaka kumi iliyopita.

Bingwa wa mbio za marathon za London Emmanuel Mutai wa Kenya, alimaliza dakika moja na sekunde 22 nyuma ya Geoffrey Mutai. Tsegaye Kabede wa Ethiopia alimaliza katika nafasi ya tatu. Geoffrey Mutai na Emmanuel Mutai hawana uhusiano wowote wa kindugu.