Waziri mkuu wa Ugiriki matatani

Bunge la Ugiriki Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Kura ya imani na waziri mkuu itafanyika

Chama cha upinzani nchini Ugiriki kimemtaka waziri mkuu George Papandreou ajiuzulu na hivyo kusambaratisha pendekezo lake la kuunda serikali ya mseto nchini humo.

Kiongozi wa upinzani Antonis Samaras pia alitangaza kuwa lazima uchaguzi ufanyike nchini humo kabla kuondoka bungeni na wajumbe wa chama chake.

Utata huo wa kisiasa umeibuka wakati bunge la Ugiriki linatarajiwa kupiga kura ya kuwa na imani na Waziri mkuu Papandreou.

Awali waziri mkuu alisema ikiwa upinzani utamuunga mkono basi atafuta mipango ya kufanya kura ya maoni kuhusu mpango wa umoja wa ulaya wa kupunguzia madeni nchi hiyo.

Kiongozi huyo anakabiliwa na upinzani mkali katika chama chake cha kisosholisti cha Pasok. Wafuasi wa chama hicho wanapinga kura hiyo ya maoni.

Chama cha Waziri mkuu Papandreou kina wabunge 152 kati ya jumla ya 300.

Wiki iliopita uamuzi wa viongozi wa ulaya wa kutoa pesa za ziada kuisaidia Ugiriki baada ya mvutano mkali ulitajwa kama mafanikio makubwa.

Lakini Bw Papandreou alizua utata hapo jumatatu baada ya kutangaza kura ya maoni itafanyika kuunga au kupinga mpango huo.

Waziri mkuu huyo alifanya mkutano wa dharura na Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkorzy na Chansela wa Ujerumani Angela Merkel ambapo viongozi hao waliamua kusimamisha mpango huo hadi matokeo ya kura hiyo yajulikane.

Kiongozi wa upinzani, Antonis Samaras sasa anahoji nia ya Bw Papandreou ya kuitisha kura hiyo ya maoni.

"Je analengo lipi, Papandreou karibu avunje nchi yetu, umoja wa ulaya na hata chama chake. Haya yote ni kwa nia ya kuniadhirisha mimi" alisema Samaras.

Migawanyiko katika chama cha waziri mkuu pia ilijitokeza wazi pale Waziri wa fedha Evangelos Venizelos aliwaelezea wabunge wa chama hicho kuwa lazima wasema kuwa hawatafanya kura ya maoni.