Damaturu Nigeria yashambuliwa

Kikundi cha wapiganaji Waislamu nchini Nigeria, Boko Haram, kimedai kuwa kilifanya mashambulio ya mabomu na risasi kaskazini mashariki mwa nchi, ambayo yameuwa watu kama 65.

Msemaji wao alilielezea gazeti moja la Nigeria, kwamba mashambulio zaidi yatafwata.

Msemaji wa Shirika la Msalaba Mwekundu aliarifu kuwa karibu mauaji yote yalitokea katika mji wa Damaturu, ambako makao makuu ya polisi yalishambuliwa na mtu aliyejitolea mhanga.

Makanisa kadha piya yalishambuliwa kwa maguruneti.

Ghasia zilianza Ijumaa katika mji ulio jirani, wa Maiduguri, ambapo kambi ya jeshi ilishambuliwa na mtu aliyejitolea mhanga.

Wakuu wa Nigeria walionya kwamba kunaweza kutokea mashambulio kabla ya sikukuu ya Idd hapo kesho.