Damaturu Nigeria sasa shuwari

Mabomu yaliyoripuliwa na Boko Haram

Wafanyakazi wa mashirika ya misaada wanasema hali sasa ni shuwari katika mji wa Damaturu, kaskazini mwa Nigeria, baada ya amri ya kafyu jana usiku.

Sasa inakisiwa kuwa watu zaidi ya 100 walikufa wakati watu waliokuwa na bunduki wa kundi la wapiganaji wenye msimamo mkali wa Boko Haram, kuvamia mji huo Ijumaa usiku. .

Katika ujumbe wake wa sikukuu ya Idd, Rais Goodluck Jonathan, aliwasihi wananchi wenzake kukana ghasia za kidini na kijamii.

Msemaji wa Shirika la Msalaba Mwekundu aliiambia BBC kwamba idadi ya watu waliouwawa katika ghasia za Ijumaa usiku, inaweza kuongezeka.

Idadi yao ya watu 63 waliokufa Damaturu, inataja wale waliofikishwa hospitali.

Lakini wakijumlishwa na wale waliozikwa na jamaa zao au kupelekwa chumba cha maiti, jumla inazidi 100.

Amri ya kutotoka nje ya jana usiku inaonesha kuwa imerejesha utulivu katika mji mkuu huo wa jimbo la Yobe.

Siku ya Ijumaa vijana wa kundi la wapiganaji wa Kiislamu, Boko Haram, walivamia mji huo ambao kawaida ni shuwari, wakiripua mabomu.

Msemaji wa kundi hilo amesema wanakusudia kuendelea kushambulia maeneo ya serikali.