Boko Haram 'kushambulia tena'.

Image caption Boko Haram wameendeleza mashambulio kama haya nchini Nigeria

Ubalozi wa Marekani nchini Nigeria umepokea taarifa za ujasusi zinazoonyesha kuwa kundi la wapiganaji wa kiislam la Boko Haram linapanga mashambulio katika mji mkuu Abuja.

Ubalozi huo umewaonya raia wake nchini humo kutotembelea hoteli za kifahari mjini humo na kutarajia vizuizi vya barabarani vinavyolindwa na jeshi.

Onyo hili limetolewa baada ya kundi hilo kutekeleza mashambulio yaliyolenga makanisa, vituo vya polisi na majengo ya serikali na kuwaua takriban watu mia moja Ijumaa iliyopita.

Baba Mtakatifu Benedict wa Kanisa Katoliki ameomba kuwa ghasia hizi zikomeshwe akisema zitachochea migawanyiko na chuki hata miongoni mwa waumini.