Wachache wajitokeza kupiga kura Liberia

Raia wachache wamejitokeza kushiriki katika duru ya pili ya uchaguzi wa urais nchini Liberia, siku moja baada ya mfuasi wa upinzani kuawa kwenye mkutano wa kampeni wa chama cha upinzani mjini Monrovia.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Polisi wa kutuliza ghasia mjini Monrovia

Katika duru ya kwanza, rais wa sasa Ellen Johnson Sirleaf alipata asilimia 44 ya kura zote.

Vyombo vya habari nchini humo vinasema milolongo michache ya watu imeshuhudiwa katika vituo vya kupiga kura mjini Monrovia na kuna hali ya wasiwasi.

Mgombea wa Upinzani Winston Tubman anasusia uchaguzi huo akidai kuwa hautakuwa wa huru na haki. Wafuasi wake waliokabiliana na maafisa wa polisi hapo jana wametishia kuvuruga shughuli za upigaji kura.

Rais Barrack Obama wa Marekani ametoa wito kwa Liberia kuendesha kura huru na ameonya dhidi ya majaribio ya kuvuruga mchakato huo.

Idadi ndogo ya wapiga kura itamaanisha kuwa Bi Ellen Johnson Sirleaf ambaye hivi majuzi alishinda tuzo ya amani ya Nobel ataongoza nchi iliyogawanyika.

Lakini ikiwa raia wa Liberia watajitokeza kwa wingi, basi atadai ushindi wa kishindo.

Wakosoaji wa Bw Tubman wanasema amejiondoa kwenye kinyanganyiro hicho kwa kuwa anahofia kushindwa na Rais Sirleaf.

Katika mji mkuu Monrovia, wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa pamoja na askari wa Liberia wanashika doria.

Miaka minane baada ya kumalizika kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe ambapo watu zaidi ya 200,000 waliuawa, mapigano mapya huenda yakasababisha Liberia kurudi tena katika machafuko.