Congo yaghadhabishwa na Tshisekedi

Kiongozi wa upinzani Tshisekedi Haki miliki ya picha vette freeze
Image caption Kiongozi wa upinzani Tshisekedi

Serikali ya Jamuhuri ya kidemokrasia ya Congo imesema kuwa vitisho vilivyotolewa na kiongozi wa upinzani Etienne Tshisekedi huenda vikachukuliwa kama uchochezi.

Bw. Tshisekedi amesema kuwa anaamini kuwa yeye ni rais na amevitaka vyombo vya utawala viliwaachie huru wafuasi wake wote waliokamatwa wakati wa vurugu za hivi karibuni.

Amewahimiza watu waingie na kuvamia magereza ikiwa watu hao hawataachiliwa kufikia leo.

Makundi ya kutetea haki za binadamu katika Jamhuri ya kidemocrasia ya congo yameonya kuhusu kuzoroka kwa hali ya usalama kabla ya uchaguzi wa tarehe 28 mwezi November.

Huu ni uchaguzi wa pili tangu kumalizika mapigano ya miaka mitano yaliohusisha pia nchi jirani. Bw. Tshisekedi aligomea uchaguzi wa mwaka 2006 akisema kuwa ulikuwa na wizi. Katika mahojiano aliyofanywa kwa njia ya simu na kituo kinachounga mkono upinzani cha RLTV siku ya Jumapili Bw.Tshisekedi mwenye umri wa miaka 78 amesema kuwa kwa masuala mengine ya utaratibu wa uchaguzi vyombo husika vinapaswa viwasiliane nae kwa kuwa kama alivyonukuliwa akisema " watu wengi wako na mimi wananiunga mkono".

"Ninatoa saa 48 kwa wafungwa wote wa upinzani waachiliwe huru.Muda huo kipita nitawataka wananchi washambulie magereza na kuwatoa wafungwa hao na kama Rais nawataka askari jela kutowazuia", alisema Tshisekedi. Siku ya Jumatatu chama cha UDPS cha Tshisekedi kilithibitisha kuwa kiongozi wao ndiye aliyefanya mahojiano hayo na kituo cha RLTV.

Maafisa wa UDPS wameiambia BBC kuwa wako tayari kuandamana hadi katika gereza kuu katika mji mkuu wa Kinshasa.

Akijibu, Waziri wa Habari Lambert Mende ameagiza kufungwa kituo cha RLTV huku uchunguzi ukisubiriwa na chombo kinachosimamia masuala ya vyombo vya habari nchini humo, tume ya uchaguzi na vyombo vya sheria.

Bw. Mende ameiambia BBC kuwa matamshi ya Tshisekedi huenda yakachukuliwa kama uchochezi.

"Tuna wasiwasi mwingi kuhusu hali ya kiongozi huyo wa UDPS huenda ana matatizo ya akili" alisema Bw. Mende.

Bw. Tshisekedi anaonekana kama mpinzani mkuu wa Rais Kabila, kuna wapinzani tisa wanaogombea kiti cha rais na wagombe wapatao 19,000 wanaogombea viti 500 vya ubunge.