Stars yaeleka Ushelisheli.

harambee stars
Image caption harambee stars

Timu ya taifa ya soka ya Kenya Harambee Stars Inaondoka nchini Kenya kuelekea nchini Ushelisheli, kwa mechi yao ya kwanza ya kufuzu kwa dimba la dunia siku ya Jumamosi.

Nahodha wa Harambee Stars Dennis Oliech amesema kuwa mechi hiyo ni mwanzo mpya kwa timu hiyo.

Oliech ambaye anaichezea klabu ya AJ Auxerre ya Ufaransa ametoa wito kwa wachezaji wenzake kusahau kushindwa kufuzu kucheza Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka ujao.

Hata hivyo Kenya itakosa huduma za mchezaji wake wa kiungo cha kati ambaye pia ni mchezaji wa Real Sociedad, McDonald Mariga.

Haki miliki ya picha Google
Image caption Mariga hatokuwepo

Mariga anauguza jeraha la mkono.

Mechi hiyo itakuwa ya kwanza kwa kocha Francis Kimanzi ambaye anarejea tena kama kocha wa Harambee Stars.

Kimanzi alichukua mahala pa Zedekiah Oteino, ambaye alifutwa kazi na wasimamizi wapya wa shirikisho la mchezo wa soka nchini Kenya, FKA ambao walichaguliwa hivi majuzi.

Akiongea kabla ya timu hiyo kuondoka Kimanzi amesema, ana imani kuwa kikosi chake kitapata matokeo mazuri.

Katika taarifa nyingine, mwanariadha wa Kenya ambaye alitoweka siku tatu zilizopita katika jimbo la Alaska nchini Marekani, kufuatia kimbunga cha theluji amepatikana akiwa hai.

Mark Cheseto, ambaye ni mwanafunzi katika chuo kikuu cha Alaska, alirejea chumbani mwake mapema siku ya Alhamisi, huku akiwa na maumivu.

Kwa mujibu wa gazeti la Daily mail, Cheseto aliripotiwa kutoweka siku ya Jumatatu hatua iliyopelekea msako mkali kuanzishwa.

Maafisa wa uokozi wakiwemo wale wanaotoa huduma za dharura katika maeneo yaliyo tanda theluji, mbwa na maafisa wengine wa ulinzi walishiriki katika operesheni hiyo ya kumtafuta Cheseto.

Afisa mkuu wa ulinzi wa chuo hicho Rick Shell, amesema haijulikani kile kilichompata mwanafunzi huyo.

Lakini mkurugenzi mkuu wa masuala ya michezo wa chuo hicho Steve Cobb amesema Cheseto kwa sasa anaendelea kupokea matibabu katika hospitali moja mjini humo.