Kura zinaendelea kuhesabiwa Liberia

Raia wa Liberia wakijiandaa kupiga kura Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Raia wa Liberia wakijiandaa kupiga kura

Idadi ya watu waliojitokeza kupiga kura katika raundi ya pili ya uchaguzi wa urais nchini Liberia, imepungua kwa kiasi kikubwa baada wa viongozi wa upinzani, kutoa wito kwa wafuasi wao kususia uchaguzi kufuatia madai ya udanganyifu na ghasia zilizotokea siku ya Jumatatu.

Mgombea wa chama cha upinzani Winston Tubman amesema amejiondoa kutoka kwa uchaguzi huo, lakini tume ya uchaguzi nchini humo, ilitoa wito kwa raia kujitokeza na kupiga kura zao.

Mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel, Ellen Johnson Sirleaf, ambaye ni mwanamke wa kwanza barani Afrika kuchaguliwa kuwa rais, ndiye mgombea wa pekee.

Mwandishi wa BBC nchini humo amesema, kuchaguliwa kwake tena, kumetiwa dosari kutokana na idadi ndogo ya watu waliojitokeza kupiga kura.

Wakati shughuli ya Kupiga kura ilipoanza mwandishi wa BBC, Jonathan Paye-Layleh alitembelea vituo kadhaa mjini Monrovia na alishuhudia watu wanane pekee wakipiga kura ikilinganishwa na mamia ya watu waliojitokeza katika awamu ya kwanza mwezi uliopita.

Ripoti zaidi zinasema kuwa idadi ndogo ya watu pia walijitokeza katika vituo vingine vya kupiga kura katika sehemu mbali mbali nchini humo,ikiwemo katika mji mkuu wa pili, Buchanan.

Vituo vya kupiga kura vilifungwa saa 12 jioni na vingine vilifungwa mapema baada ya kubainika kuwa hakuna wapiga kura zaidi ambao wangejitokeza.

Raia wengi wanasema kuwa hawakuona haja ya kupiga kura tena baada ya kuonekana kuwa Bi Sirleaf alikuwa akielekea kushinda awamu nyingine.

Sirleaf alichaguliwa kuwa rais mwaka wa 2005, katika uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia tangu kumalizika kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka 14.

Siku ya Jumatatu usiku, maafisa wa polisi waliokuwa wamejihami walivamia na kufunga vituo viwili vya radio, Kituo cha Kings FM kinachomilikiwa na mgombea mwenza wa Tubman ambaye ni mchezaji wa soka mashuhuri wa zamani George Weah.

Kituo kingine kilichofungwa ni kituo cha Love FM, kinachomilikiwa na mwanasiasa wa upinzani Benoni Urey, ambaye chama chake cha National Patriotic Party (NPP) kinashirikiana na chama cha CDC.