Malema wa ANC asimamishwa uanachama

Chama tawala nchini Afrika Kusini, ANC kimefukuza kiongozi wa vijana Julius Malema kutoka cheo chake kwa muda wa miaka mitano.

Hii ni baada ya kamati ya nidhamu kumpata na hatia ya kuvunjia chama heshima.

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Analazimika kuondoka ANC

Julius Malema ambaye hakuwepo kwenye makao makuu ya chama chake wakati hukumu hiyo ilipotolewa, amepewa siku 14 kukata rufaa ya uamuzi huo.

Mwenyekiti wa kamati ya nidhamu Derek Hanekom, amesema kuwa tabia ya Malema imeishushia hadhi chama cha ANC na sio njia muafaka ya kuelezea hisia za kutoridhika na sera za chama.

Kamati hiyo imempata na hatia ya kuvuruga mkutano wa ANC, kukivunjia hadhi chama hicho kwa kudai mageuzi ya utawala nchini Botswana na kuchochea migawanyiko chamani.

Viongozi wengine wa umoja wa vijana, miongoni mwao msemaji Floyd Shivambu, pia wamefukuza kutoka kwa nyadhifa zao kwa muda wa miaka mitatu.

"Tabia ya Malema itaharibu uhusiano wa kimataifa wa chama chetu na kuvunjia heshima Afrika Kusini kwa jumla na sio vyema kuwa ivumiliwe" alisema Bw Hanekom.

Hata hivyo kamati hiyo haikumpata Malema na hatia kwenye kosa la kuchochea ubaguzi wa rangi.

Wadadisi wa siasa nchini Afrika Kusini wanasema uamuzi huu unaweza kuwa ushindi kwa Rais Jacob Zuma ambaye anakabiliwa na upinzani kutoka kundi linalopendelea sera za kutaifisha uchumi wa nchi hiyo, ikiwemo kunyakuwa ardhi za wazungu.

Malema anaushawishi mkubwa miongoni mwa vijana na watu masikini na wadadisi wanasema ikiwa hata kata rufaa huenda harakati zake zikawa changamoto kubwa kwa chama cha ANC.