Kiongozi wa upinzani arudi Congo

Haki miliki ya picha vette freeze
Image caption Bw Tshisekedi

Kiongozi mkuu katika makundi ya upinzani nchini Congo, Ettiene Tshisekedi amerejea katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kutoka ziara ya Afrika ya kusini, akizidisha hofu ya machafuko ya kisiasa kabla ya uchaguzi mkuu baadaye mwezi huu kuanzia tarehe 28 Novemba.

Tume ya uchaguzi imeitisha Mahakama ya Kimataifa inayosimamia makosa ya jinai isimamie uwezekano wa kutokea uonevu katika kipindi cha uchaguzi.

Baada ya ndege yake kutua, Bw Tshisekedi alikariri matamshi aliyoyatoa mapema kupitia mahojiano na kituo cha televisheni ya nchini Congo kwa simu, akisema kuwa alisema hivyo kutokana na umaarufu alionao unaomfanya ajihisi kuwa ni rais.

Vile vile kiongozi huyo aliutaja utawala wa sasa wa nchi hiyo kuwa ni wa kidikteta na kuwataka wafuasi wake wajibize vitendo vya unyanyasaji wanaotendewa.

Wakuu wa serikali ya Congo wamemsimamisha mtangazaji aliyepitisha mahojiano ya Bw Tshisekedi huku mashirika ya kutetea haki za binadamu yakionya kuwa ghasia huenda zikazuka ikiwa viongozi wataushuku mchakato wa uchaguzi salama.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Kinshasa rais wa tume ya uchaguzi, Daniel Ngoy Mulunda, amesema anamheshimu Bw Tshisekedi lakini akaonya ghasia za kisiasa zinaweza kufikia viwango visivyohitajika, na kiongozi huyo alitaja jinsi wafuasi wa upinzani walivyomuandama.

Ngoy Mulunda ameitaka mahakama ya kimataifa inayohusika na makosa ya jinai itume wajumbe wa kusimamia uchaguzi na kuiomba iwachukulie hatua wale watakaokiuka sheria na kuzusha ghasia.

Tume hiyo ya uchaguzi pia imetangaza kamati ya maridhiano iliyoundwa na viongozi wa makundi ya viongozi wa dini na wanawake wasaidie mjadala baina ya viongozi wa kisiasa wakati wa kipindi hiki cha uchaguzi.