Maharamia wa Kisomali kizimbani Ufaransa

Washukiwa Haki miliki ya picha TONY KARUMBAAFPGetty Images
Image caption Washukiwa wa uharamia

Watu sita wamepelekwa mahakamani mjini Paris, Ufaransa kwa tuhuma za kushambulia chombo cha baharini Septemba 2008, katika kesi ya kwanza nchini Ufaransa kushtaki washukiwa wa uharamia wa Kisomali.

Watu hao wanashtakiwa kwa utekaji nyara wa chombo na watu na kufanya wizi wa kutumia silaha baada ya kudaiwa kuteka boti na watu wake, ambao ni mtu na mke wake wote wenye umri wa miaka 60.

Mizigo

Majeshi maalum ya Ufaransa yalivamia chombo hicho kwenye pwani ya Somalia, na kuwaachilia huru mateka hao. Mshukiwa wa saba wa uharamia aliuawa.

Mawakili wa utetezi wanasema washukiwa hao walilazimishwa kufanya kitendo hicho.

Maharamia wameteka meli nyingi katika pwani ya Somalia, hasa za mizigo.

Wanajeshi maalum

Washukiwa hao wakiwa na umri wa kati ya miaka 21 hadi 35, wanakabiliwa na adhabu ya kifungo cha kwenda jela maisha, iwapo watakutwa na hatia.

Washukiwa hao wanatuhumiwa kushambulia chombo kiitwacho Carre d'As tarahe 2 Septemba 2008 na kudai kikombozi cha dola milioni 2, ili kuwaachilia huru raia hao wa Ufaransa Jean-Yves na Bernadette Delanne.

Chombo hicho pamoja na wamiliki wake waliachiliwa huru na wanajeshi maalum wa Ufaransa wiki mbili baadaye.

Hawajakamatwa

Wakili wa mmoja wa washukiwa amesema mshukiwa huyo ambaye hakutajwa jina, kuwa ni mvuvi na alilazimishwa kushiriki katika shambulio hilo kwa sababu yeye ni baharia.

Wakili mwingine wa utetezi amesema waliopanga shambulio hilo bado hawajakamatwa.

Washukiwa wa Kisomali katika kesi nyingine tatu za uharamia nchini Ufaransa wanasubiri kufikishwa mahakamani.

Shirika la Mabaharia la Kimataifa limesema doria na kutengemaa kwa hali ya usalama mwaka huu kumepunguza utekaji nyara unaofanywa na maharamia wa Kisomali.

Utafiti uliofanywa nchini Marekani uligundua kuwa uharamia unagharimu uchumi wa dunia dola bilioni 7 hadi 12 kila mwaka.