Mugabe na Tsvangirai kumaliza ghasia

Mugabe Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Mugabe na Tsvangirai wamekubaliana kumaliza ghasia

Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe na Waziri Mkuu Morgan Tsvangirai wametoa wito wa kuvumiliana kufuatia mvutano kuongezea wakati uchaguzi ukikaribia.

"Tunataka kuishi katika nchi tulivu," Bw Mugabe amesema, baada ya mazungumzo na Bw Tsvangirai, hasimu wake wa muda mrefu.

Chama cha Bw Tsvangirai cha MDC kimerejea kuwatuhumu wanamgambo wanaomuunga mkono Bw Mugabe kwa kuvuruga mikutano yake ya hadhara.

Uchaguzi unatarajiwa mwakani, kumaliza serikali ya muungano iliyoundwa mwaka 2009.

Viongozi hao wawili walitia saini makubaliano ya kushirikiana kufuatia uchaguzi ulioleta utata, ambao Bw Tsvangirai aliamua kujiondoa katika raundi ya pili dhidi ya Bw Mugabe, akitoa sababu za kuwepo kwa ghasia za kisiasa.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Tsvangirai kupambana na Mugabe tena mwakani

Muungano wao umekuwa ukizongwa na kutoelewana.

Baada ya kukutana na Bw Mugabe mjini Harare, Bw Tsvangirai ametoa wito kwa majeshi ya usalama kutofanya ghasia na kuruhusu chama chake kufanya mikutano, limeripoti shirika la habari la AFP.

"Natoa wito kwa vyombo vya dola kuanza kuchukua majukumu yao ya kitaifa kwa makini," amekaririwa akisema.

"Vyombo vya dola, hasa polisi, lazima walinde watu na sio kuwadhuru."

Bw Mugabe amesema vyama viruhusiwe kufanya mikutano kwa uhuru.

"Tunaunganishwa pamoja na utaifa wetu, tunaimba wimbo mmoja wa taifa" alikaririwa akisema.

"Ikiwa tuliafikiana na wazungu [wakati wa uhuru 1980] sasa sisi wenyewe weusi, kwanini tunahangaishana, kwa nini tunapigana?"

Siku ya Jumapili, chama cha Bw Tsvangirai cha MDC kilisema wafuasi wa chama cha Bw Mugabe cha Zanu-PF kilirwarushia mawe nje ya mji wa Harare.

MDC inasema hilo ni tukio la hivi karibuni la Zanu-PF kuharibu shughuli zake kabal ay uchaguzi.

Pia kimetuhumu polisi kwa kurusha mabomu ya machozi katika makao yake makuu wiki iliyopita.

Tarehe ya uchaguzi haijatajwa bado, ambapo wawili hao wanatarajiwa kupambana tena, kwa mara nyingine.