Berlusconi ang'atuka

Rais wa Utaliana, Giorgio Napolitano, ameanza kufanya mashauriano juu ya namna ya kuunda serikali mpya, baada ya Waziri Mkuu, Silvio Berlusconi, kujiuzulu.

Haki miliki ya picha AFP

Mjumbe wa zamani wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Mario Monti, ndiye aliyeelekea kuteuliwa kuongoza nchi, na kuisaidia Utaliana kupambana na madeni yake mengi.

Bwana Berlusconi - ambaye ameongoza Utaliana kwa muda mrefu kabisa tangu Vita vya Pili vya Dunia - kama alivoahidi, aliondoka jana usiku, baada ya bunge kukubali mpango wa kuimarisha uchumi wa nchi.

Kwenye barabara za mji wa Rome alishangiliwa na kwengine kuzomewa na kuitwa mpumbavu.

Mwanasiasa huyu ni bilioneya aliyeandamwa na kashfa wakati wa uongozi wake, lakini aliweza kushikilia madaraka.

Baraza la senate limeshakubali mpango mpya wa uchumi, na bunge linatarajiwa kufwata leo, au kesho.

Kati ya hatua zitazochukuliwa ni kuzidisha umri ambapo Wataliana wanaweza kustaafu, kupandisha bei ya mafuta, mabadiliko katika kodi za mapato, na mali ya taifa itauzwa.

Bwana Berlusconi aliahidi kung'atuka pale mpango huo ukishapitishwa na bunge, na mwanasiasa huyo aliyeongoza siasa za Utaliana kwa karibu miongo miwili, inafikiriwa atarithiwa na Mario Monti.

Bwana Monti ni mwana uchumi anayeheshimiwa na anaonekana kuwa mtu atayefaa kushika hatamu wakati huu wa msukosuko wa kiuchumi.