Syria yalalamikia nchi za Kiarabu

Syria imetoa wito kufanywe mkutano wa dharura wa viongozi wa nchi za Kiarabu, kujadili ghasia za nchi hiyo.

Haki miliki ya picha Reuters

Imesema hayo siku moja baada ya Jumuia ya nchi za Kiarabu kusimamisha kwa muda uanachama wa Syria, kwa kushindwa kutekeleza mpango wa amani uliopendekezwa na jumuia hiyo.

Syria imeiomba jumuia kutuma ujumbe wa mawaziri, kusimamia utekelezaji wa mpango huo. Na maelfu ya Wasyria wanaandamana dhidi ya uamuzi wa Jumuia ya nchi za Kiarabu, kusimamisha uanachama wa nchi hiyo.

Televisheni ya taifa inaonesha picha za umati wa watu katika miji ya Damascus, Aleppo, na Latakia, uliobeba picha za Rais Bashar al-Assad, na mabiramu yanayolaani Jumuia ya nchi za Kiarabu.

Huku nyuma, katika mji wa Hama, wanaharakati wanasema wanajeshi wamewapiga risasi waandamanaji ambao wakipiga kelele dhidi ya serikali, kwenye maandamano yaliyotayarishwa na serikali.

Na Misri imesema inapinga kabisa majeshi ya nchi za nje kuingilia kati nchini Syria, kwa kisingizio chochote kile.

Taarifa ya wizara ya mashauri ya nchi za nje ya Misri ilitoa wito kwa Syria, kutekeleza mapendekezo ya Jumuiya nchi za Kiarabu.