Marekani yakerwa na thamani ya yuan

Rais Obama amemwambia rais wa Uchina, Hu Jintao, kwamba Marekani haiwezi kuvumilia zaidi na ina hamu kuwa Uchina ibadilishe sera zake za kiuchumi.

Haki miliki ya picha AFP

Marais hao walizungumza hayo kando ya mkutano wa kilele wa Jumuiya ya Asia na Pacific, APEC, kisiwani Hawaii.

Mwandishi wa BBC mjini Beijing, anasema mazungumzo ya kinaga-naga namna hivo kati ya viongozi hao ni nadra; na inaonesha Rais Obama, hakumficha Rais Hu Jintao, fikra zake.

Marekani imekuwa ikidai kwa muda mrefu kuwa thamani ya sarafu ya Uchina, yuan, iko chini - na hivo inaipa Uchina nafuu inapouza bidhaa zake nchi za nje.

Inaarifiwa kuwa Bwana Hu alijibu kuwa matatizo ya biashara na ukosefu wa ajira wa Marekani, hayatanufaika hata sarafu ya Uchina ikipandishwa sana.