Mahasimu wa Urais DRC wakutana Goma

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Rais Joseph Kabila anawania tena Urais wa DRC

Chama kikuu cha Upinzani cha UDPS kilichosimamisha mgombea katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo kimeomba tume ya uchaguzi nchini humo kumfuta katika nafasi ya Ugombea Rais Joseph Kabila kwa madai kuwa amekiuka katiba.

Chama hicho kinamtuhumu Rais Kabila kutumia mali na majengo ya serikali kufanya kampeni zake.

Chama hicho cha UDPS kimesimamisha mgombea wake Etienne Tshisekedi kuchuana na Rais Joseph Kabila katika uchaguzi unaofanyika mwishoni mwa mwezi huu, Novemba 28.

Katika mfululizo wa kampeni zao nchini DRC mahasimu hao Rais Joseph Kabila na Etienne Tshisekedi Jumatatu walitarajiwa mikutano yao ya kampeni katika mji wa mashariki wa Goma.

Hali hiyo inaonekana kuzusha wasiwasi wa kutokea machafuko kati ya wafuasi wa wagombea hawa wawili.

Mwandishi BBC Idhaa ya Kiswahili aliyeko Kinshasa Patrice Chitera anasema upinzani unamshutumu Rais Kabila kutumia mali za serikali ikiwemo pesa na kutumia helkopta za jeshi la Taifa.

Msemaji wa chama cha UDPS Bw Kalembelembe amesema chama chao kimetoa wito huo baada ya kuona kuwa katika kampeni za Rais Kabila picha zake zimewekwa kwenye majengo ya serikali na pia matumizi ya viwanja vya soka vya umma.

Hatua hiyo ya upinzani imekuja siku moja baada ya muungano wa vyama vinavyomuunga mkono Rais Kabila kuanza kuondoa picha za Rais Kabila kwenye uwanja wa Kandanda.

Baadhi ya viongozi wa vyama vinavyomuunga mkono Rais Kabila wamesema barua ya UDPS ni kisingizio cha kufanya uchaguzi usifanyike.

Kampeni za kuwania kiti cha Urais nchini DRC zinaendelea wakati Rais Kabila aliripotiwa kuwa katika mkoa wa Katanga na baadaye alitarajiwa kuingia mjini Goma mchana wa Jumattatu.

Mwandishi wa BBC anasema wafuasi wa wagombea wote walikuwa wakiwasubiri mahasimu hao wawili katika uwanja ndege wa Goma huku duru zikisema kuwa Rais Kabila angewasili mjini humo jioni ya Jumatatu.