Eriterea kutuma ujumbe maalum Kenya

Rais wa Eriterea

Huku harakati za Jeshi la Kenya ndani ya Somalia zikiingia mwezi mmoja sasa kuwasaka wapiganaji wa Al-Shabaab, ujumbe wa juu kutoka Eriterea unatarajiwa mjini Nairobi hii leo.

Kenya imekuwa ikilaumu Eriterea kwa kuwafadhili wanamgambo hao wa Kiisilamu nchini Somalia. Hata hivyo nchi hiyo imekanusha kuwapa silaha wanamgambo hao na hata kutangaza kuunga mkono hatua za Kenya kuwasaka wapiganaji hao ndani ya Somalia.

Hivi Maajuzi Kenya ilitishia kukatiza uhusiano wake na Eriterea kulalamikia ushirikiano kati ya utawala wa Asmara na wanamgambo wa Al Shabaab ambao wanapigana na serikali ya mpito ya Somalia.

Kutokana na mvutano huo Kenya imekuwa mbioni kutafuta uungwaji mkono kanda ya Afrika kutokana na harakati zake pamoja na kushinikiza Eriterea kuwekewa vikwazo.

Ili kuepuka kuendelea kutengwa Eriterea imemtuma Waziri wake wa Mambo ya nje mjini Nairobi ili kuelezea uhusiano wake na kundi hilo.

Kenya ilianzisha harakati za kijeshi ndani ya Somalia kuwasaka wanamgambo wa Al Shabaab ambao wametuhumiwa kuhatarisha usalama wa Kenya kufuatia visa vya utekaji nyara wa raia wa kigeni.