Mwandishi akataa tuzo Nigeria

Mwandishi Riwaya Chinua Achebe Haki miliki ya picha other
Image caption Mwandishi Riwaya Chinua Achebe

Mwandishi mashuhuri wa riwaya nchini Nigeria,Chinua Achebe amekataa kupokea mojawapo ya tuzo kubwa za heshima za Nigeria.

Hii ni mara yake ya pili kufanya hivyo akisema matatizo yale yale yaliomfanya asikubali tuzo hiyo miaka saba iliyopita bado yamesalia.

Chinua Achebe ni mojawapo wa magwiji wa Afrika katika utunzi wa hadithi na riwaya ambaye sifa zake zimeenea duniani kote. Kwa hiyo matamshi yake yana uzito mkubwa. Alipokataa tuzo kuu ya heshima ya kamanda wa Jamhuri ya Shirikisho la Nigeria mnamo mwaka 2004 alilalamika kwamba nchi yake inageuzwa kuwa himaya iliyozama katika ufisadi na vurugu.

Akiikataa kwa mara ya pili tuzo hiyo alisema matatizo yale yale bado yapo hayajashughulikiwa seuze kusuluhishwa. Rais wa Nigeria Goodluck Jonathan ameelezea mshangao na masikitiko yake kwa uamuzi huo. Rais huyo amesema anatumai kwamba Bwana Achebe atapata fursa ya kuizuru Nigeria kutoka Marekani anakoishi na kuona jinsi serikali ya Nigeria inavyozidi kupiga hatua.