Waandamana kupinga ubakaji Cameroon

Image caption Rais wa Cameroon Paul Biya

Maelfu ya wanawake wamekataa kufanya kazi kwenye mashamba kaskazini magharibi mwa Cameroon mji wa Wum baada ya matukio ya ubakaji na mashambulizi kutoka kwa wafugaji wa ng’ombe.

Wanawake wansema wasichana ni miongoni mwa watu walioathirika na mwanamke mmoja alikufa kutokana na majeraha Jumatatu usiku, mwandishi wa BBC Randy Joe Sa'ah aliyeko Wum anaripoti.

Kundi la wanawake limeandamana kupinga vitendo hivyo mbele ya ikulu ua kiongozi wa kimila kudai ulinzi, anasema.

Eneo hilo limeathiriwa na migogoro ya ardhi kati ya jamii zinazopingana.

Maafisa wa serikali wameitisha mkutano Jumanne mjini Wum kujadili tatizo hilo.

Watuhumiwa kupigwa

Binti wa miaka 11 kutoka kabila la Aghem mwandishi wa BBC anaripoti aliponea chupuchupu kubakwa na wafugaji wawili kutoka kundi la Akuh

"Kwanza walinipiga halafu wakatishia kunikata vipande vipande kwa kutumia panga kama ningepiga kelele. Baadaye mmoja wao akanichania chupi na kuchana gauni yangu," alisema.

"Halafu wakanikandamiza chini na kujaribu kunningilia kwa nguvu"

Binti huyo alipata bahati ya kutobakwa wakati wanaume wawili walipokuja kumwokoa.

Mdogo wake wa miaka minne aliwaambia waandishi kuwa aliweza kukimbia kabla hajakamatwa na watuhumiwa hao wa ubakaji.

"Nilikwenda kwa dada yangu kuchukua viazu. Nikawaona wafugaji aho. Nikamjulisha dada yangu na kumwambia kukimbia. Alitupa mzigo wake lakini akakamatwa. Nikakimbia nyumbani kumwambia mama yangu kuwa mdogo wangu amekamatwa na wafuga ng’ombe," alisema.

Mwandishi wa BBC anasema wanaume waliokasirishwa na vitendo hivyo waliwatafuta watuhumiwa hao wanne na kuwapiga vibaya na sasa wanatibiwa hospitali majeraha yao.

Mwandishi wa BBC anasema alikutana na mmoja wa watuhumiwa hao akiwa amefungwa ping katika kitanda cha hospitali chini ya ulinzi wa polisi.

"Kundi la watu lilinituhumu kumbaka binti lakini sikuwa nimefanya hivyo. Muda huo nilikuwa nimelala," mtuhumiwa amemwabia mwandishi

"Nilichukuliwa na kundi la vijana ambao walinipiga vibaya. Halafu wakanikabidhi kwa polisi"

Kundi kubwa la wanawake wameandamana kupinga nje ya ikulu ya kiongozi wa kimila wa Aghem, Bah-ambi III, kwa siku ya nne kuonyesha hasira zao juu ya ubakaji huo na kutaka ulinzi.

Jamii mbili zinaishi kwa amani katika eneop hilo lakini wakati mwingine ugomvi huzuka kuhusu haki za maeneo ya kuchungia.