Waasi washambulia kambi ya kijeshi Syria

Raia wa Syria katika mkutano wa Rais Assad hii leo Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Raia wa Syria katika mkutano wa Rais Assad hii leo

Kundi la upinzani la Syria, limesema kuwa wanajeshi waasi wa Syria-FSA- wameshambulia kambi kuu ya kijeshi karibu na Mji Mkuu wa Damascus.

Sehemu ya jengo la idara ya ujasusi ya kikosi kikali cha angani huko Harasta inasemakana imeharibiwa lakini hakuna taarifa za majeruhi.

Haya ndio mashambulio makubwa sana ya FSA tangu vuguvugu la kuipinga serikali ya Syria kuanza.

Mashambulio hayo yametokea kabla ya mkutano wa dharura wa Jumuiya ya Kiarabu kufanyika nchini Morocco kujadili njia za kukomesha umwagikaji damu . Uturuki ambayo sio mwanachama wa Jumuiya hiyo, inahudhuria mkutano huo na imesema Syria italipa yanayotendeka kwa gharama kubwa.

Serikali ya Syria imeweka vikwazo vikali kwa waandishi wa kigeni na hii inasababisha taarifa zote za ghasia kutoweza kuthibitishwa kwa uharihisi.

Umoja wa Mataifa unasema kuwa zaidi ya watu 3,500 wameuawa tangu vuguvugu la kudai mapinduzi kuanza nchini humo mwezi Marchi. Kwa upande wake serikali ya Syria inalaumu magenge yalio na silaha na wakereketwa kusababisha ghasia hizo.

Maelfu kadhaa ya watu walihudhuria mikutano mjini Damascus na Latikia kuonesha kumuunga mkono Rais Bashar al Assad.

Mikutano hii ilikuwa ya kuadhimisha siku baba yake Assad, Hafez al-Assad, alipotwaa mamlaka mwaka 1970.

Baraza la kitaifa la Syria (SNC) -ikiwa ni mseto wa makundi ya upinzani -ambalo liko nchini Uturuki limesema mashambulio dhidi ya Harasta yamefanywa na wanajeshi waasi wa FSA.

Mashambulio kama hayo yataonekana kuwa na kishindo kikubwa kwa kuwa idara ya ujasusi ya jeshi la angani la Syria inafahamika na kuogopewa kati ya idara za serikali zinazotikisha na kuogopewa na imehusika sana katika kuwakandamiza waandamanaji dhidi ya Bw. Assad.

Hili ndiyo shambulio ambalo ndio kubwa zaidi kuwahi kufanywa na FSA.

Wanaharakati wanasema kuwa wanajeshi waasi hao walishambulia jengo hilo kutoka sehemu tatu. Ndege za Helkopta ambazo inadhaniwa ni za serikali zimeonekana katika eneo hilo.

Mkazi mmoja wa Harasta ameliambia shirika la habari la Reuters: " Nilisikia milipuko kadhaa na vile vile sauti za ufyatulianaji risasi"

Kamati za uratibu za eneo hilo pia zimetaja mashambulio hayo ilhali kikundi cha kushughulikia haki za binadamu Syria kilichoko Uingereza kimesema kumekuwa na mashambulio mengine Zamalke, Hamuriya na Douma.

Kwa mujibu wa taarifa za shirika la habari la AFP tawi la Khaled ibn Walid la FSA - lililoko katika mji wa Homs ambao ndio chimbuko la ghasia- katika taarifa yake limesema limefurahia mashambulio hayo.

"Tunawapa pongezi ndugu zetu, waasi mashujaa na Mungu aibaraki mikono yenu kwa operesheni zenu za alfajiri za kulishambulia jengo la ujasusi la Harasta" taarifa yao iliongeza.

Kundi la FSA liliundwa na waasi waliompinga Bw. Assad miezi michache iliyopita na linadai kuwa na wanachama 15,000 kufikia katikati ya mwezi october lakini linachukuliwa kama uwongezaji chumvi.

Kamanda wa kundi hilo, Riyad al-Asad, amekuwa Uturuki kwa miezi michache iliyopita lakini anasemakana amerejea Syria kuongoza harakati zao.