Watoto wauawa Somalia, yasema UNICEF

Ramani ya Somalia

Shirika la Umoja wa Mataifa linalosimamia maslahi ya watoto- UNICEF limesema kwamba takriban watoto 24 waliuawa na wengine 50 kujeruhiwa katika vita nchini Somalia mwezi wa Oktoba pekee .

Ripoti ya UNICEF inasema idadi hiyo imeendelea kuongezeka na kuufanya mwezi huo kuwa mbaya zaidi kwa watoto.

Ripoti mpya iliyotolewa shirika la Watoto la Umoja wa mataifa inasema watoto wengi nchini Somalia wanauawa au kujeruhiwa wakati katika uwanja wa vita. Mwaka huu pekee zaidi ya watoto100 wameangamia.

Shirika hilo pia linasema zaidi ya watoto 600 wamesajiliwa kuwa wanajeshi huku mia mbili ya watoto wa kike wakiwa wamebakwa.

Nchi ya Somalia imekuwa vitani kwa miongo miwili sasa. Mapigano zaidi yamechacha baada ya majeshi ya Kenya kuingia nchini humo kukabiliana na wanamgambo wa Al Shabaab.

Hata hivyo jeshi la Kenya halijalaumiwa kusababisha maafa au majeruhi ya watoto.

Mwakilishi wa UNICEF nchini Somalia Sakinder Khan amesema idadi ya watoto wanaoendelea kufa na kujeruhiwa nchini Somalia itaendelea.

Hii ni kutokana na hatua ya wanamgambo kuendelea na usajili wa watoto katika kambi zao.

Shirika la UNICEF ni moja wapo mashirika chache ya kimatifa ambayo yamepenya kusini mwa Somalia katika shughuli za kutoa misaada. Maeneo ya kusini yanadhibitiwa na wanamgambo wa Al Shabaab.

Wakati huo huo imedhibitishwa mulipuko wa kipundupindu katika kambi ya wakimbizi wa somalia kaskazini mwa Kenya.

Shirika la Kimataifa la Wakimbizi UNHCR limesema mtu mmoja amefariki kutokana na maambukizi.